Askofu Shoo aomba msamaha

04Jul 2020
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Askofu Shoo aomba msamaha

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo, amewaomba msamaha Watanzania waliouguliwa na kupoteza ndugu, jamaa na marafiki kwa ugonjwa wa corona kutokana na kunyanyapaliwa na kukimbiwa na baadhi ya madaktari, wauguzi na viongozi wa kanisa.

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Frederick Shoo:PICHA NA MTANDAO

Vilevile, kiongozi huyo wa kanisa ametoa msaada wa vifaa kinga na dawa vyenye thamani ya Sh. milioni 100 kwa hospitali 24 nchini zinazomilikiwa na kanisa hilo, ili ziendelee kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wa corona na kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Akizungumza jijini Arusha jana, wakati akikabidhi msaada huo kwa wawakilishji wa hospitali hizo nchini, alishukuru Shirika la Kimataifa la Act Alliance kwa kutoa fedha zilizowezesha kununua vifaa tiba kwa ajili ya kukinga madaktari na wauguzi pamoja na dawa za aina mbalimbali za kukabiliana na corona na magonjwa mengine.

“Lakini, tangu janga hili lizuke katika Mji wa Wuhan, China na baadaye kuingia Tanzania Machi mwaka huu, wengi tuliingia hofu na hata baadhi ya hospitali kukimbia wagonjwa na baadhi yetu sisi viongozi wa dini tulishindwa kutoa huduma ya ibada kwa waliofariki, ni kutokana na kuogopa kuambukiwa, ninaomba sana msamaha kwa ajili ya hili,” alisema.

Askofu Shoo alisema binadamu wote wanastahili huduma za kibinadamu na kuzikwa kwa heshima hata kama amefariki dunia kwa ugonjwa hatari, hivyo waliokumbwa na unyanyapaa wa aina yoyote, anawaomba msamaha kwa niaba ya kanisa.

Alishauri hospitali zote nchini kujiweka tayari kukabiliana na majanga ya magonjwa yoyote yanapotokea kama corona kwa kuwa na vifaa mbalimbali vya kuhudumia Watanzania.

"Katika ugonjwa huu, tuliona na tulipata funzo kuwa hata ukiwa na fedha nyingi, bila Mungu hakuna kitu na hapa ninampongeza na kumwombea Rais John Magufuli kwa kusimama kidete kuondoa watu hofu na kusisitiza kumwomba Mungu,” alisema.

Dk. Shoo pia alitoa wito kwa serikali kuwatafuta na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote wanaojihusisha na ukatili dhidi ya watoto katika familia na majumbani hasa wanafunzi wanaopewa mimba na kukatishwa ndoto zao.

Aliwashauri viongozi wa dini  wawe mstari wa mbele kuwafariji na kuwapa ushauri nasaha wale wote walioathrika na corona, kwa kuwa ugonjwa huo bado upo na kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari zote kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na serikali.

“Niwatie moyo wafanyabiashara ambao mitaji yao imeyumba wakati  wa corona, kwamba sasa hali yetu inaelekea kurejea kama kawaida, ninawaombea kwa Mungu awainue upya waendelee na biashara zao  kwa nguvu na kuujenga uchumi wetu na familia zao,” alisema.

Aliwapongeza madaktari na wauguzi kwa kufanya kazi wakati huo mgumu wa janga la corona, huku baadhi yao wakipata vikwazo vya kutolipwa mishahara yao.

Dk. Shoo pia alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuongoza vema serikali yake na kufanikiwa kutangazwa na Benki ya Dunia kuwa Tanzania sasa imefikia uchumi wa kati.

"Rais alipoingia katika serikali hii, alisema Watanzania tufanye kazi, ili tufikishe taifa katika uchumi wa kati, lakini katika hili baadhi ya watu walibeza kuwa haiwezekani na kusema ni ndoto, lakini limewezekana na Benki ya Dunia imetutangaza rasmi kuingia katika uchumi wa kati, ninampongeza sana Rais,” alisifu.

Katibu Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Braghtony Killewa, alisema wakati wa corona, baadhi ya hospitali zilipata vikwazo vya uhaba wa watumishi baada ya baadhi yao kuugua na kuwekwa kambini.

“Kutokana na hili, baadhi ya hospitali zilijikuta zina upungufu wa watumishi, lakini mlipambana na kuhudumia wagonjwa, kweli Mungu awabariki sana kwa moyo huo,” alisema.

Mkuruegzni wa Programu za Afya wa KKKT Tanzania, Dk. Paul Mmbando, alitaja baadhi ya vifaa na dawa zilizokabidhiwa jana kwa hospitali hizo kuwa ni barakoa za kitabibu maboksi 200, buti jozi 300, paracetamol za watoto na wakubwa makopo 200, dawa za mafua, vitakasa mikono madumu 400 ya lita tano kila moja.

Vingine ni dawa za Vitamini C makopo 2400, Enthromicyin na vingine vinavyosaidia kupambana na ugonjwa huo.

Habari Kubwa