Askofu wa Tanzanite afariki dunia

22May 2019
Na Waandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Askofu wa Tanzanite afariki dunia

MFANYABIASHARA maarufu wa madini mkoani Arusha, Thomas Mollel maarufu kama ‘Askofu’, amefariki dunia ghafla jijini Dodoma.

MFANYABIASHARA maarufu wa madini mkoani Arusha, Thomas Mollel maarufu kama ‘Askofu’,.

Askofu alikuwa jijini Dodoma kwa ajili ya kushuhudia kuapiswa kwa mbunge mteule wa jimbo la Arumeru Mashariki, Dk. John Pallangyo, ambaye aliapishwa jana bungeni.

 

 

 

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Meru, Shaaban Mdoe ambaye ni miongoni mwa ujumbe wa mbunge mteule Dk. Pallangyo uliosafiri kwenda Dodoma, jana alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

 

Mdoe ambaye pia ni katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, alisema walipokea taarifa ya kuugua kwa Askofu muda mfupi baada ya kuachana naye na kurejea katika hoteli aliyofikia baada ya wote kupata chakula cha jioni.

 

"Tulikuja wote juzi yeye akiwa katika gari lake binafsi na sisi katika usafiri wetu mwingine kumsindikiza mbunge mpya wa jimbo la Arumeru Mashariki, Dk. Pallangyo Bungeni tushuhudie akiapishwa leo, ambayo mwenzetu katangulia kabla ya siku hiyo,"alisema.

 

Alisema waliongozana naye akiwa kama Mjumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya Meru na Mei 20 majira ya saa 3:00 usiku walikuwa pamoja kwenye hotel moja jijini humo walikula chakula pamoja akiwa hana shida yeyote.

 

“Tulikaa pale na aliagiza soda Club Soda tu na alipomaliza saa nne usiku huo aliondoka na kwenda hoteli alipofikia lakini kufika saa tano usiku nilipokea simu toka kwa Mwenyekiti wa wazazi wilayani kwangu, akinitaarifu Askofu ameanguka hotelini anakimbizwa hospitalini," alisema.

“Tulipigiwa simu na mkewe kwamba amezidiwa baada ya kuteleza akitoka kuoga, lakini tulipofika hospitali Mkoa wa Dodoma muda mfupi baadaye tulijulishwa kwamba amefariki,” alisema Mdoe.

 

Askofu alikuwa miongoni mwa wachimbaji wachache wa madini waliofanikiwa na akaendelea kuishi katika kijiji alichozaliwa cha Mbuguni wilayani Arumeru, kilometa chache kutoka ilipo migodi ya madini ya Tanzanite katika eneo la Mirerani.

 

Alikuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Meru na pia mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM katika wilaya hiyo. Kati ya mwaka 2010 na 2015 alikuwa diwani wa kata ya Mbuguni

 

Askofu atakumbukwa zaidi kwa tukio la mwaka 1995 baada ya kupata madini ya Tanzanite aligawa fedha kwa kuzirusha akiwa ghorofani katika jengo lake la Hoteli ya Pallsons iliyopo katikati ya Jiji la Arusha.

 

Akizungumzia kifo hicho, mchimbaji wa madini ya Tanzanite huko Mererani, Rahim Massawe, alisema kimewagusa wengi kwa kuwa alisaidia watu wengi kufanikiwa kuingia kwenye uchimbaji wa madini.

 

“Kazi ya kuchimba madini inahitaji mtaji kwa ajili ya kununua vifaa mfano baruti, diseli na chakula cha wafanyakazi huku ukiendelea kuchimba kwa muda mrefu bila kupata madini lakini askofu alikuwa msaada katika kuwawezesha wengi wasikwame,” alisema.

 

Naye aliyewahi kuwa kiongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wilayani Arumeru na sasa yupo makao makuu ya chama hicho jijini Dodoma, Lothi Nassele, alisema anamkumbuka Askofu kama mtu mwenye ushawishi mkubwa ndani ya jamii.

 

Mbali na kuwa mchimbaji wa madini na mwanasiasa, Askofu pia alikuwa mwana michezo ambaye alifanikiwa kuanzisha timu ya soka ya Pallson iliyofanikiwa kucheza ligi kuu ya soka ikiwa na makazi yake katika kijiji cha Mbuguni.

 

Afisa habari wa shirikisho la wachimbaji wa Madini nchini (Femata), Dk. Bernard Joseph alisema wachimbaji wamempoteza rafiki, mpambanaji na mtu muhimu kwenye sekta hiyo.

 

"Wakati wa uhai wake alikuwa na mapenzi mema na vijana kwani alianzisha timu ya mpira wa miguu ya Pallsons ambayo ilifikia hatua kubwa kwenye soka," alisema Dk. Joseph.

 

Naye, mmiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite, Fatuma Kikuyu, alisema wachimbaji madini wamepata pigo kubwa kwani Mollel alikuwa anasaidia wachimbaji wenzake ambao hawakuzalisha madini.

 

Alisema ni pengo kubwa wamepata wachimbaji madini ya Tanzanite kwani watu kama Mollel wapo wachache kutokana na kuwajali wachimbaji wenzao.

 

Mchimbaji wa madini ya Tanzanite, Haji Msham Ngokwe, alisema sekta ya madini imepoteza mtu muhimu kwani Mollel ni miongoni mwa matajiri wa mwanzo mwanzo kupata madini ya Tanzanite.

 

"Huyu alikuwa na roho nzuri hadi watu wakamuita Askofu badala ya Mollel. Alisababisha wengine waione Sh.milioni moja kutokana na kuwa na roho ya utoaji," alisema Ngokwe.

 

Kwa mujibu wa Katibu huyo, madaktari walikuwa wanaufanyia uchunguzi mwili wa Askofu na baadaye kusafirishwa kwenda nyumbani kwake mkoani Arusha kwa mazishi.

 

 

 

Imeandikwa na Novatus Makunga na Cynthia Mwilolezi, ARUSHA

 

Habari Kubwa