Ataka mikakati ya ulinzi miundombinu

07Mar 2020
Julieth Mkireri
Kisarawe
Nipashe
Ataka mikakati ya ulinzi miundombinu

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kuweka mikakati madhubuti itakayosaidia kulinda miundombinu ya umeme.

NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, picha mtandao

Pia amesema mikakati hiyo itakayoambatana na ulinzi itakuwa msaada kuondoa vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikilisababishia hasara taifa.

Mgalu alitoa agizo hilo jana kutokana na kukithiri kwa matakio ya uhujumu wa miundombinu ya umeme ikiwamo wizi wa mafuta na uharibifu wa Transfoma unaofanywa na watu wasio na nia njema kwa taifa.

Akizungumza akati wa uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kata ya Manerumango wilayani Kisarawe, Mgalu alisema ili kukabiliana na uhujumu wa miundombinu ya umeme, kunatakiwa kuwapo mikakati ya kuidhibiti.

"Ni wazi kuwa iko haja kuwapo mikakati ya kudhibiti vitendo hivi ambavyo vimekuwa vinakwamisha azma ya serikali ya kuwapatia umeme wananchi wake kwa wakati na maeneo ambayo tayari wameunganishiwa wanakosa nishati hiyo kutokana na kundi la watu wachache wasiopenda maendeleo," alisema Mgalu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme katika hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Kisarawe, Mhandisi Nyanda Busumabu, alielezea mikakati itakayowezesha vijiji vyote wilayani hapa kufikiwa na umeme ifikapo Juni, mwakani.

Busumabu alisema uunganishaji wa nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ya Kisarawe utasaidia kufungua wigo wa wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo la kimkakati ambalo liko karibu na jiji la Dar es Salam na Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere (Selous).

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, alisema uwapo wa ofisi hiyo utasaidia kusogeza huduma karibu kwa wananchi na pia itarahisisha upatikanaji wa taarifa pindi linapotokea tatizo na hatimaye kushughulikiwa kwa haraka.

Mmoja wa wakazi wa Manerumango, Idd Konde, aliishukuru serikali kwa uwapo wa ofisi hiyo karibu na wananchi ambayo itawapunguzia kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma Kisarawe.

Habari Kubwa