Ataka vyeti dhamana mikopo kwa vijana

24May 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Ataka vyeti dhamana mikopo kwa vijana

MBUNGE wa Momba (Chadema), David Silinde, ameitaka serikali ishauriane na taasisi za kifedha, wanafunzi wa vyuo vikuu watumie vyeti vyao vya elimu ya juu kukopa ili kujiajiri.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Silinde alihoji kutokana na  ukosefu wa ajira, serikali ina mkakati gani wa wahitimu hao kujiajiri kwa kushauriana na taasisi hizo ili kupata mikopo kwa njia hiyo.                      “Na pia ni kwa nini serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wasigawe ardhi kwa wanafunzi wote wanaomaliza vyuo vikuu ili wajiajiri kwa kufanya hizo kazi na baada ya hapo warejeshe mikopo yao,”alihoji. Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, alisema katika taasisi za kifedha moja ya masharti ya mtu kupata mkopo ni uwasilishaji wa dhamana. “Asilimia kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu bado hawana dhamana ndiyo maana sisi kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tumeona ni njia pekee ya kuwasaidia vijana. Kwa kuanzia, tunachokifanya ni kuwahamasisha kukaa kwenye vikundi na kuwawezesha kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kiuchumi,”alisema. Alisema baraza hilo lina mifuko takribani 19 ya uwezeshaji inayotoa mikopo na ruzuku ambayo ina ukwasi wa Sh. trilioni 1.3. Aliwataka wahitimu kutumia mifuko ya uwezeshaji kwa kuwa ina riba nafuu na pia inaweza kubadilisha maisha yao. Pia alisema takribani ekari 200,000 zimetengwa kwa ajili ya vijana nchini. Katika swali la msingi, Silinde alitaka kujua mkakati wa serikali wa kuongeza ajira kwa Watanzania waliohitimu vyuo bila kujali kada walizosomea lakini mpaka sasa wako mtaani. Akijibu swali hilo, Mavunde alisema serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa programu ya taifa ya kukuza ujuzi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha vijana kuajirika. Alisema lengo la programu pia ni kupunguza tofauti ya ujuzi iliyopo kati ya nguvukazi na mahitaji ya soko la ajira. Aidha alisema katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo wanapata ajira za kuajiriwa na kujiajiri na serikali imeendelea kuandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza fursa za ajira. Alitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda nchini kupitia sekta binafsi kwa lengo la kutengeneza nafasi nyingi za ajira. “Utekelezaji wa miradi mikubwa nchini ikiwamo mradi wa bomba la mafuta, ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa nishati kupitia miradi mbalimbali ambayo yote kwa ujumla, itasaidia kupanua wigo wa nafasi za ajira,”alisema. Mavunde alisema pia kuhimiza halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi kwa ajili ya vijana kila mkoa. “Kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana,”alisema Naibu Waziri huyo alisema pia kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na masuala ya ajira kwa lengo la kuwaongezea ufahamu mpana katika masuala ya ajira na kuwaongezea uwezo wa kujiamini katika kujiajiri kupitia sekta mbalimbali.   

Habari Kubwa