Athari 6 kiuchumi za corona kwa SADC hizi

14Jul 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Athari 6 kiuchumi za corona kwa SADC hizi

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema corona imeleta athari sita za kiuchumi kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Akifungua kikao cha siku tatu cha maofisa waandamizi wa hazina na Benki Kuu ndani ya Jumuiya hiyo, alisema athari hizo zimegusa sekta mbalimbali.

Alizitaja ni kushuka kwa mauzo nje, kudorora kwa sekta za huruma na kuongezeka kwa madeni ya serikali hizo.

Nyingine ni kupungua kwa shughuli za kiuchumi, kuongezeka idadi ya wakopaji wanaoshindwa kurejesha mikopo katika sekta za fedha na kupungua kwa mapato ya ndani ya serikali.

James ambaye ni Mwenyekiti wa Maofisa Waandamizi wa Hazina wa SADC, alisema corona imeleta changamoto mpya katika kupiga hatua za maendeleo ya uchumi hasa katika kufikia malengo ya viashiria vya uchumi mpana katika Jumuiya.

“Ili kukabiliana na athari hizo, kuna haja ya nchi wanachama kutumia mifumo ya kitaasisi katika kutafuta njia mbadala zenye ubunifu, ili kuharakisha hatua za kuimarisha uchumi wa ndani ya Jumuiya.

“Kikao hiki ni njia muafaka katika kujadili changamoto za kiuchumi na kutoa mapendekezo ya kitaalam yatakayowezesha mikutano ya kamati ya mawaziri wa fedha na uwekezaji na magavana wa benki kuu,” alisema.

Pia alisema changamoto nyingine ni utakatishaji fedha haramu na ufadhili wa makundi ya kijangili.

“Tatizo hili limesababisha baadhi ya nchi wanachama kuingia katika orodha ya nchi zilizo kwenye athari ya kuingia kwenye vikwazo vya kimataifa kwa kushindwa kutimiza vigezo na masharti ya Kikosi cha Masuala ya Fedha,” alisema.

Alisema hali hiyo inaweza kusababisha kudorora kwa jitihada za kuvutia uwekezaji na kuathiri malengo ya jumuiya.

“Ninaziomba nchi wanachama kuungana kwa pamoja na kufanya uchunguzi wa namna ambavyo tutaweza kuzuia na kuondokana na tatizo hili kwa kushauriana na kubadilisha uzoefu ili kupata ufumbuzi wa tatizo hili,” alisema.

Kadhalika, alisema pamoja na mafanikio ya kiuchumi ndani ya Jumuiya, baadhi ya nchi hivi karibuni zimeendelea kukabiliwa na changamoto ya ukuaji mdogo wa uchumi, kuongezeka kwa nakisi ya bajeti, kupungua kwa mapato ya serikali na kuongezeka kwa madeni yanayotishia utekelezaji wa azma ya maendeleo katika jumuiya.

Kuhusu mkutano huo ambao utakuwa wa siku tatu kuanzia jana, alisema utakuwa na ajenda sita na kuzitaja baadhi kuwa ni kupitia taarifa ya maendeleo ya sekta ya fedha ya magavana wa benki kuu.

“Kupitia taarifa ya utekelezaji wa masuala ya udhibiti wa fedha haramu, kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maandalizi ya Miradi ya Maendeleo wa SADC.

“Kupata taarifa ya hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa Mfuko Maalum wa Kugharamia Miradi ya Miundombinu ya Usafirishaji wa Nishati ya Umeme, inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).”

Pia, alisema ajenda nyingine ni kupitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji uliofanyika Windhoek, Namibia mwezi Julai mwaka jana.

Kadhalika, alisema watapokea na kujadili taarifa ya hatua iliyofikiwa ya namna ya uendeshaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC.

James alimshukuru Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa SADC, kwa kusimamia kwa ufanisi shughuli za jumuiya ikiwamo suala la fedha na uwekezaji.

Pia, alizipongeza baadhi ya nchi wanachama kwa uamuzi wao wa kufungua na kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi wakati wanaendelea kuwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya corona.

Habari Kubwa