Auawa, ang'olewa meno mwili watupwa mtoni

23Mar 2017
Ibrahim Yassin
ILEJE
Nipashe
Auawa, ang'olewa meno mwili watupwa mtoni

MKAZI wa Kata ya Isansa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe (jina limehifadhiwa) anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 53, amekutwa amekufa na mwili wake kutupwa Mto Mwala umbali wa mita 300 kutoka nyumbani kwake.

Aidha, watu waliomuua, pia walimng'oa meno yake.

Wakizungumza jana na gazeti hili, baadhi ya wakazi wa eneo hilo, walisema waliuona mwili huo wakati wakitoka kuchota maji mtoni na kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya kijiji.

Walisema uongozi wa kijiji ulitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio wakiwa na daktari.

Sunuba Silupumbe, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, alidai kuwa wakati wa uhai wake, marehemu alituhumiwa kupenda kutembea na wake za watu.

"Ilifikia hatua ya kuonywa na watu wa aina mbalimbali pasipo mafanikio hadi jana (juzi), walipomkuta ameuawa na mwili wake kutupwa kando ya mto huo.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Mathias Nyange, alisema polisi walikwenda eneo la tukio baada ya kupewa taarifa na serikali ya kijiji na kuukuta mwili huo ukiwa pembezoni mwa Mto Mwala huku ukiwa hauna meno na na majeraha kidevuni.

Kamanda Nyange alisema chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi kwakuwa marehemu wakati wa uhai wake, alikuwa akituhumiwa kutembea na wake za watu.

Alisema mbinu iliyotumika ni kumvizia akiwa njiani akielekea nyumbani kwake akitoka matembezini nyakati za usiku na kumuua.

Hata hivyo, Kamanda Nyange aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa na badala yake wawafikishe mbele ya vyombo vya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Aliongeza kuwa baada ya uchunguzi wa kipolisi na kitabibu, waliiruhusu familia na ndugu kuuchukua mwili huo kwa maziko.

Kamanda Nyange alisema hakuna mtu au watu waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo na upelelezi unaendelea.

Habari Kubwa