Auawa na polisi akidaiwa jambazi

18Mar 2019
Steven William
  MUHEZA
Nipashe
Auawa na polisi akidaiwa jambazi

JESHI la Polisi wilayani Muheza mkoani Tanga limemuua kwa kumpiga risasi Mkazi wa Dar es Salaam, Mwinyiheri Nuhu, likidai alikuwa anajihusisha na ujambazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alidai jana kuwa Nuhu alikuwa miongoni mwa watuhumiwa wanne wa ujambazi waliovamia nyumba ya mfanyabiashara Ally Nassoro wilayani Muheza wakiwa na bunduki juzi usiku.

Alisema tukio la kuuawa kwa mtuhumiwa huyo wa ujambazi lilitokea juzi usiku saa nne usiku katika Kijiji cha Songa wilayani humo ambako mfanyabiashara huyo anaishi.

Kamanda Bukombe alidai watuhumiwa hao wa ujambazi walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara huyo wakitumia gari ndogo na kupora Sh. milioni moja zilizokuwako.

Alidai kuwa wakati watuhumiwa hao wakiendelea kufanya uhalifu, askari polisi kutoka vituo vya Wilaya ya Muheza na Hale wilayani Korogwe, walifika kwenye nyumba hiyo na kuanza kupambana nao kwa kurushiana risasi.

Kamanda Bukombe alidai kuwa wakati wakirushiana risasi, polisi walimuua Nuhu, lakini wenzake walitoroka na wanaendelea kusakwa na jeshi hilo.

Alidai walinasa bunduki mbili, kitambulisho cha Nuhu na Sh. milioni moja zilizokuwa zimeporwa kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Habari Kubwa