Aweso ataka ushiriki wananchi usomaji wa mita za maji

10Aug 2020
Neema Hussein
KATAVI
Nipashe
Aweso ataka ushiriki wananchi usomaji wa mita za maji

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso amezitaka Mamlaka za Maji nchini Kuwashirikisha Wananchi wanaotumia huduma ya maji pale wanapokwenda kusoma mita ili kuepuka malalamiko ya wananchi hao kuzidishiwa bili.

Naibu waziri wa maji Juma Aweso akifungua maji katika bomba la maji lililopo majalila Halmashauri ya Tanganyika Mkoani Katavi.

Aweso ameyasema hayo leo Agosti 10,2020 alipofanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maji mkoani Katavi likiwemo tenki la maji linalojengwa katika mtaa wa Mapinduzi Manispaa ya Mpanda ambalo litakamilika Septemba 15 mwaka huu.

Alisema ikitokea mwananchi akasitishiwa huduma ya maji na kulipa bili aliyokuwa anadaiwa inatakiwa arudishiwe huduma hiyo ndani ya saa 24, na mtu anapotaka kuunganishiwa maji amelipia bili za kuunganishiwa inatakiwa ndani ya siku saba mtu huyo apate maji.

Naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso akikagua tenki la maji linalojengwa katika Mtaa wa Mapinduzi Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Saleh Muhando akimtua mama ndoo ya maji kichwani.

Alisema wameleta fedha zaidi ya  billioni 5.6 katika Mkoa wa Katavi  kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji vijijini na tayari miradi 19 inatekelezwa katika Halmashauri zote tano kwa mkoa huo ambapo katika Wilaya ya Tanganyika Serikali imetoa billion 1.3.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mpanda, Mhandishi Iddo Richard alisema mradi wa maji wa Ikolongo ukikamilika utasaidia kupunguza mgao wa maji na wananchi wa Mpanda watapata maji kwa asilimia 60.

Wananchi wa Tanganyika wamemshukuru Rais Magufuli na viongozi wote wa Serikali kwa kutatua changamoto ya maji na sasa wananchi hao wanapata maji muda wote.

Habari Kubwa