Azaki zajengewa uwezo ulipaji kodi

01Dec 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Azaki zajengewa uwezo ulipaji kodi

ASASI za kiraia mkoani Shinyanga, zimepewa mafunzo namna ya kulipa kodi ili kuongeza mapato ya Serikali.

Afisa elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga Justine Katiti akitoa elimu namna ya kulipa Kodi kwa Asasi za kiraia mkoani Shinyanga.

Mafunzo hayo yametolewa leo mjini Shinyanga, kwa kushirikisha Asasi za kiraia 50, mafunzo ambayo yamefadhiliwa na Shirika la Foundation for Civili Society, pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACONGO).

Afisa elimu kwa mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga Justine Katiti, alisema Asasi za kiraia zinapaswa kuwa zinalipa kodi Serikalini, kupitia Michango ya wanachama, Misaada, zawadi, kodi ya pango, pamoja na vyanzo vyao vingine vya mapato.

Alisema Asasi za kiraia ni walipa kodi kama walipa kodi wengine, ambapo wanapaswa kujisajili (TRA) ili kupata TIN namba, na kuanza kulipa kodi hiyo ya Serikali kupitia shughuli zao mbalimbali ambazo huzitekeleza ndani ya jamii.

“Kiwango cha ulipaji kodi kwa Asasi za kiraia ni asilimia 30 ya mapato yao kila mwaka, mara baada ya kutoa gharama za uendeshaji, na mnatakiwa kupeleka taarifa ya makato ya kodi ya mishahara kila mwezi ndani ya siku Saba,” alisema Katiti.

“Kodi ndiyo chanzo kikubwa cha mapato Serikalini, hivyo naziomba Asasi za kiraia mlipe kodi kwa wakati, ili kuisaidia Serikali kupata fedha za kuendesha shughuli zake mbalimbali,”aliongeza.

Naye mgeni Rasmi kwenye mafunzo hayo Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Zuwena Omary, alizitaja Asasi hizo za kiraia kujenga utamaduni wa kulipa kodi mara baada ya kupewa mafunzo hayo, huku akizitaka pia ziwe zinawasilisha mpango kazi wao wa miaka mitatu Serikalini ili waone namna ya kufanyanao kazi.

Pia alizitaka Asasi hizo, pale zinapokuwa zinatekeleza majukumu yao ndani ya jamii wahakikishe wanatoa matokea chanya kwa kupunguza changamoto ama kumaliza kabisa matatizo ambayo huwakabili wananchi kwa mradi ambao wanautekeleza.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwamo Mathias Chidama kutoka Shirika la CHIDEP, walisema hawakuwahi kupata mafunzo hayo ya ulipaji kodi kwa Asasi za kiraia ndiyo mara ya kwanza, na kutoa ushauri pale watakapokwama wapewe maelekezo zaidi na elimu hiyo iwe ya mara kwa mara..

Kwa upande wake Afisa Program Mwandamizi kutoka Shirika la Foundation For Civil Society Ofisi ndogo ya Dodoma Nicholaus Mhozya, alisema wameendesha mafunzo hayo kwa Asasi za kiraia mkoani Shinyanga, ili kuwajengea uwezo katika masuala ya kisheria, pamoja na ulipaji kodi ya Serikali ili wafanye shughuli zao bila ya bughuza

Habari Kubwa