Azaki zalia na Sheria ya Takwimu

06Dec 2018
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Azaki zalia na Sheria ya Takwimu


ASASI za Kiraia (Azaki) zimesema zimeichambua Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2018 na kubaini dosari nne ambazo zinapaswa kurekebishwa, ili kutoathiri kazi za utafiti zinazofanywa na wadau kwa maendeleo ya nchi.


mkurungenzi mkuu ofisi ya takwimu dk albina chuwa, picha na mtandao

Akisoma tamko la Azaki mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Mtandao Policy Forum, Japhet Makongo, alisema upungufu walioubani upo katika vipengele vinavyohusu maana ya takwimu rasmi, usambazaji wa takwimu, makosa na adhabu pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhodhi mamlaka ya kuzalisha taarifa za kitakwimu.


Alisema kuwa pamoja na kutambua umuhimu wa sheria hiyo ambayo inalenga kuzuia usambazaji na uchapishaji wa taarifa zinazoweza kupotosha umma, wanaona kuna haja ya kuifanyia marekebisho wakiamini kuiacha kama ilivyo, kutaathiri kwa kiwango kikubwa utafiti wenye manufaa kwa maendeleo ya taifa.


Alisema Kifungu cha Tatu cha sheria hiyo kinatoa tafsiri mpya yenye maana ya takwimu rasmi zilizoandaliwa, kudhibitishwa, kukusanywa au kusambazwa kwa idhini ya NBS lakini haijazingatia jukumu na wajibu wa wadau wengine ambao pia wanazalisha takwimu hususan Azaki na wadau mbalimbali wa maendeleo.


Alisema vifungu vya tatu na 18 vya sheria hiyo vimeipa NBS mamlaka makubwa ya kukusanya na kutoa takwimu rasmi na kwamba vifungu hivyo vinakwenda kinyume cha Mkataba wa Afrika wa Takwimu wa Mwaka 2009 unaotafsiri mamlaka za takwimu kama taasisi za kitaifa za takwimu au taasisi nyingine zinazosimamia uzalishaji na usambazaji wa takwimu hizo katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa.


"Vifungu hivyo vimeongeza urasimu kwenye mchakato mzima wa kukusanya na kusambaza takwimu na kuleta vikwazo visivyokuwa na ulazima katika kupata takwimu muhimu. Na sheria hii haijaainisha kipindi maalum cha NBS kushughulikia maombi ya vibali vya kufanya tafiti, wala haijainisha utaratibu maalum wa maombi ya vibali," alisema Makongo na kuongeza:


“Sheria hii imerundika majukumu kwa NBS ya kusimamisha takwimu kutoka vitengo vyote vya serikali pamoja na wadau wengine. Mzigo huu unaweza kuathiri utendaji kazi wa ofisi hii.

Na pia, sheria haina utaratibu wa kukata rufaa endapo mwombaji akinyimwa kibali cha kuchakata na kusambaza taarifa za kitakwimu, jambo ambalo ni kinyume na Katiba.

"
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Hebron Mwakagenda, alisema Azaki hizo zinaona ni vema sheria hiyo ikafanyiwa marekebisho kwa kuzingatia Ibara ya 18 ya Katiba inayowapa wananchi haki ya kutafuta, kupata na kusambaza taarifa pamoja na umuhimu wake katika maendeleo ya nchi.


Alisema wanapendekeza makosa ya adhabu chini ya sheria hiyo yajikite katika kusimamia mchakato wa upatikanaji na usambazaji wa takwimu rasmi na siyo takwimu zote kwa kuwa makosa ya adhabu zinazohusiana na upotoshaji wa taarifa nyingine unashughulikiwa na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na sheria nyingine.


"Sheria itambue uwapo wa taasisi na wadau wanaoandaa takwimu huru ambazo ni mbadala wa takwimu rasmi ili kuwezesha kuwapo kwa mjadala hai na chanya kwa maendeleo," alisema.


Mwakagenda pia alisema ni vema sheria ikaondoa sharti la kuomba vibali zaidi ya mara moja kwenye kuandaa, kukusanya na kusambaza takwimu rasmi na kufanyia marekebisho kifungu kinachoruhusu adhabu.


“Sheria iweke ukomo wa adhabu ili iendane na nadharia ya msingi ya kutoa adhabu hiyo na kuepusha uwezekano wa utoaji wa adhabu kinyume cha haki za binadamu na kuondoa takwimu zisizo rasmi kwenye adhabu kwani sheria hii inahusu takwimu rasmi," alisema.


Mwakagenda alisema ni muhimu sheria iongezwe kifungu kinachowezesha wadau kukata rufaa pale maombi yao ya vibali yanapokataliwa au kutoridhika na uamuzi ya NBS na ielekeze ofisi hiyo kutoa sababu ya kutokubali vibali kwa waombaji.
*Soma tamko la azaki hizo ukurasa wa tano

Habari Kubwa