Azaki zatishia kuishtaki serikali

11Dec 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Azaki zatishia kuishtaki serikali

ASASI za kiraia (Azaki) zimesema endapo serikali haitafanya maboresho katika kanuni za uendeshaji wa Azaki nchini, zitalazimika kuifikisha mahakamani, zikidai kanuni hizo zina masharti magumu kuyatekeleza.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na  Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa, wadau 150 wa mashirika ya asasi za kiraia walipokutana kujadili na kupitia kanuni mpya za uendeshaji wa Azaki zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Alisema Azaki zitabinywa na kanuni hizo na hawapo tayari kupeleka mikataba yao kwa Msajili wa Hazina na hata kueleza taarifa zao za fedha kwenye magazeti.

"Uwazi ni jambo zuri lakini siyo kila kitu cha kuweka katika gazeti," alisema, "hili la kuweka taarifa kwenye gazeti ni gharama.

"Kupeleka mikataba kwa Msajili wa Hazina ni utaratibu ambao hauwezi kutusaidia chochote, hapa ni kuturudisha nyuma ama kuua asasi za kiraia."

Olengurumwa alisema sheria hizo ambazo wamewekewa hawajashirikishwa, hivyo ni vizuri kwa serikali kukaa pamoja katika kufanya maboresho na siyo kuwakandamiza katika utendaji wao wa kazi.

"Kama hawatafanyia kazi maboresho hayo, tutakwenda kuihoji mahakama uhalali wa kutulazimisha sisi kupeleka mikataba kwa Msajili wa Hazina," alisema.

Aliongeza kuwa sheria mpya ya mwaka 2018 inawataka kuwasilisha mikataba yao kwa Msajili wa Hazina pamoja na mambo mengine ambayo alidai ni kandamizi dhidi ya asasi za kiraia.

Alisema ni vizuri wizara na wadau wa asasi za kiraia kukaa kwa pamoja kufanya maboresho katika kanuni hizo, vinginevyo serikali inakwenda kuua taasisi zisizo za kiserikali.

Alisema kanuni ni nzuri lakini kuna baadhi ya vifungu vinawafunga kufanya kazi katika mazingira magumu na upatikanaji wa rasilimali utakuwa mgumu kwao.

Alisema asasi za kiraia ni wabia wa wadau wa maendeleo, hivyo wanapowekewa mazingira magumu kunasababisha taifa kukosa fedha za kigeni na taifa kukosa asasi zinazoajiri kwa kuwa wanatoa ajira kwa asilimia kubwa ya Watanzania.

“Leo hapa tunaandaa mapendekezo yetu ambayo kimsingi tutayawasilisha wayafanyie kazi maana kuna mambo mengine hayatekelezeki na endapo tukashindwa kuelewana njia ya mwisho ni kwenda mahakamani,” alisema. 

“Kama mapendekezo yetu yakikataliwa tutarudi tena kukutana na wanasheria wetu. Mahakama ni chombo ambacho kinatoa haki, hatuna njia nyingine, tutakwenda mahakamani kuwauliza hizi kanuni ni haki ya kikatiba na watatoa uamuzi lakini tusingependa kufikia huko."

Alisema kanuni hizo zina makosa mengi ya kijinai, akitolea mfano kwamba ukiacha tu kutoa taarifa ya ukaguzi wa fedha ni moja ya makosa hayo.

“Makosa mengi ya jinai yameanzishwa katika hizi kanuni walizotupatia, watu wengi ama mashirika watafungwa na hizi kanuni,” alisema Olengurumwa.

“Ukitaka serikali ikuamulie hela yako uitumie vipi, uhuru wa kufanya kazi haupo, tutakuwa tena siyo taasisi isiyo ya kiserikali.

"Mashirika ya serikali ndiyo yanatakiwa kwenda kwa Msajili wa Hazina, sisi ni mashirika yasiyo ya kiserikali, tuna utaratibu wetu tayari tumeshasajiliwa na tunawajibika na fedha zetu zinatoka kwa wadau.

“Mikataba yetu ni kwa ajili ya wadau wetu tuliokubalina pamoja na msajili wetu wa asasi za kiraia, sasa kutupeleka tena kwa Msajili wa Hazina halafu ndiyo aanze kuturuhusu, hii inaonyesha hali siyo nzuri, hiki kipengele tunataka kitoke."

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kutetea Haki za Kisiasa na Uraia, Demokrasia na Utawala Bora, Jimmy Luhende, alisema serikali imependekeza kuwapo kwa sheria za asasi za kiraia.

Alisema baada ya mkutano huo kumalizika watakutana na serikali ili kuieleza upungufu uliopo katika kanuni hizo kwa kuwa zinawazuia kufanya kazi yao muhimu ya kuikosoa serikali.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Uraia na Msaada wa Kisheria, Charles Odelo, alisema kanuni zinakwenda kinyume cha sheria mama ya asasi za kiraia ya mwaka 2002.

Habari Kubwa