Azimio kumpongeza JPM laligawa Bunge

14Jun 2018
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Azimio kumpongeza JPM laligawa Bunge

BUNGE limepitisha azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuundeleza mji wa Dodoma na kuupa hadhi ya jiji huku wabunge wa upinzani wakipinga uamuzi huo.

RAIS JOHN MAGUFULI (KULIA) Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), (KUSHOTO).

Wabunge hao wa upinzani wamepinga uamuzi huo wakiitaka serikali kuandaa kwanza mazingira ya miundombinu kabla ya kutangaza kuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi.

Akisoma azimio hilo bungeni jijini Dodona jana, Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (CCM), alisema kitendo cha kuupa mji wa Dodoma hadhi ya jiji kitaleta manufaa makubwa kwa kuwa hata mgawanyo wa rasilimali utaongezeka.

Aliwaomba wabunge kuitaka serikali kukamilisha haraka mchakato wa kuuleta bungeni muswada huo.

“Bunge hili katika mkutano wake wa 11 kikao cha 50, linaazimia kumpongeza Rais Magufuli.

 

Hivyo, tunaiomba serikali kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali itakayoendana na hadhi ya makao makuu na jiji kama vile ujenzi wa barabara zenye kiwango, miundombinu ya majisafi na majitaka, upimaji na upangaji mzuri wa Jiji la Dodoma," alisema. 

Baada ya Simbachawene kutoa hoja hiyo, wabunge wote wa CCM walisimama kuunga mkono azimio hilo, lakini jambo hilo halikuungwa mkono na wabunge wa upande wa upinzani ambao wote hawakusimama.Katika kujadili azimio hilo, Mbunge wa Temeke, Abdalah Mtolea (CUF), alisema lilipaswa kutanguliwa na maombi ya fedha kwa ajili ya uboreshaji wa mji wa Dodoma.

“Tulitegemea mngeishawishi serikali itenge fedha kwa ajili ya kutimiza hivyo vigezo kwa sababu sasa hivi Dodoma haina hata stendi kuu ya mabasi ya mikoani.

“Wabunge wa Dodoma mjipange, tumieni fursa serikali itenge fedha ili kujenga miundombinu na si hii ‘blabla’ tunayoifanya," alisema mtaalamu huyo wa sheria.

Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CUF), aliihoji serikali kinachotangulia kati ya vigezo na sheria.

“Hakuna anayepinga Dodoma kuwa makao makuu au jiji, lakini ni kipi kinatangulia kati ya sheria na vigezo vya kuwa jiji,” alisema Kuchauka.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Ditopile (CCM), aliunga mkono azimio hilo huku akiahidi kuwa wananchi wa Dodoma watampa ushindi mkubwa Rais Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.

“Tumelipokea hili na tunajua mwaka 2020 kuna mtanange, lakini tutashinda kwa asilimia kubwa. Kama kuna mtu hajaunga mkono hili, ajue kuwa tutashinda," alisema Ditopile.

Mbunge wa Moshi Vijijini, Antony Komu (Chadema), alisema: “Mpango huu wa kuifanya Dodoma kuwa jiji ni wa kukurupuka. Moshi ilipaswa kuwa jiji, lakini imenyimwa kwa sababu fulani fulani. Kuna watu wamemshauri vibaya Rais.”

 

  Mbunge wa Viti Maalum, Munde Tambwe (CCM), alisema azimio hilo linapaswa kuungwa mkono ikizingatiwa kuwa Rais Magufuli amefanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi, hivyo anastahili kupongezwa.

“Anastahili pongezi kwa kweli. Ndege, reli, amegawa tablets kwa walimu wa shule za msingi na vingine vingi. Naunga mkono hoja hii ya Simbachawene,” alisema.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, aliunga mkono hoja hiyo, akieleza hata Wajerumani walipokuja Tanganyika, waliiteua Bagamoyo kuwa makao makuu yao na ilikuwa na nyumba moja tu.

“Uamuzi wa kuitangaza Dodoma kuwa jiji ni muhimu. Sasa tunaangalia vizuri maana ni mji mkuu ambao uko katikati ya Tanzania,” alisema Dk. Mwakyembe na kuongeza:

“(Saed) Kubenea (Mbunge wa Ubungo- Chadema), anasema usafiri wa Dodoma si rahisi. Safiri kidogo Kubenea, nenda Kampala uone hali ya usafiri.”Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Selemani Jafo, alisema serikali imetenga Sh. bilioni 35 kwa Jiji la Dodoma kujenga na kuimarisha miundombinu yake.

“Niwaombe wabunge wenzangu, tuishi kwa upendo, kauli zetu zisiwafadhaishe wenyeji wa Dodoma,” alisema na kufafanua zaidi:

“Sisi viongozi tuliopewa dhamana tukikaza mishipa kana kwamba jambo hili si jema, tunawanyong’onyesha wananchi.

“Tumetenga zaidi ya Sh. bilioni 35 kujenga soko, stendi ya kisasa na barabara za ndani. Tunataka Dodoma iwe the ‘best city’ (jiji bora zaidi) kwa Afrika Mashariki kwa mipango miji.

“Tunataka Dodoma uwe mji mzuri zaidi. Hata unaposhuka kwa ndege, Dodoma ni tofauti na unavyoshuka Morogoro na miji mingine nchini.

“Rais hakukurupuka kufanya uamuzi huu. Moshi ina kilomita za mraba 58, kama Moshi ni km za mraba 58, kila jambo linakwenda kwa mujibu wa sheria.”

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema uamuzi wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na kuipa hadhi ya jiji si wa kukurupuka kwa kuwa umo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

“Ilani ya CCM iliielekeza serikali ndani ya miaka mitano ihakikishe imehamisha makao makuu ya serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma,” alisema.

Mhagama aliongeza: “Ilani inaitaka serikali ihakikishe majengo ya serikali yajengwe Dodoma na tumeanza kujenga na viwanja vyote vipimwe na tayari tumeanza.

“Tunavyohamishia Dodoma tumetekeleza kwa vitendo nia ya Baba wa Taifa. Kati ya wafanyakazi 7,440 wa wizara zote wanaotakiwa tumebakiza 909 tu ambao hawajahamia hapa. Wengine wote wamehamia Dodoma.

“Baada ya kuhamia wote Dodoma, hapatakuwa na tatizo la miundombinu kama wanavyodai baadhi ya wabunge.” 

Habari Kubwa