Azua taharuki akidai kujifungua mnyama karunguyeye

17Sep 2021
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
Azua taharuki akidai kujifungua mnyama karunguyeye

KATIKA hali isiyo ya kawaida, mkazi wa mtaa wa Butiama, mji wa Bariadi Regina Frednand (46), amedai kujifungua mnyama aina ya karunguyeye na kuzua taharuki kwenye eneo hilo.

Akiongea na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake jana na kukuta umati wa watu uliofika kushuhudia tukio hilo, mama huyo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita Agosti 12, 2021.

Regina alisema majira ya saa 1:10 asubuhi wakati akijiandaa kwenda kwenye ibada ya kwanza kanisani, gafla alijisikia maumivu makali tumboni na ndipo akaelekea chooni kujisaidia.

“Baada ya kufika chooni huku nikiwa na maumivu makali, haja ambayo nilikuwa nikisia haikutoka…cha kushangaza nilisikia maumivu makali sehemu za siri na kuhisi kuna kitu kinaning’ata,” alisema Regina.

“Kadiri maumivu yalivyoongezeka nikajisikia kusukuma ndipo kikatoka kitu ambacho sikukielewa…nikapiga kelele kuomba msaada kwa watoto wangu ambao naishi nao hapa, baada ya kufika walikitazama na kubaini kuwa alikuwa panyabuku, baadaye wakakimwagia maji ya baraka ndipo kilipogeuka na kuwa mnyama aina ya karunguyeye,” alieleza Regina.

Alipoulizwa kama alikuwa mjamzito, Regina alikiri kuwa na ujauzito wa miezi mitano ambao aliupima mwenyewe nyumbani kwa kutumia kipimo cha mkono alichonunua duka la dawa.

Hata hivyo, alisema hakuwahi kwenda kliniki kwa madai kuwa alikuwa anasubiri ujauzito ufikishe miezi sita ndipo tukio hilo lilitokea kabla ya kuanza kliniki.

“Baada ya tukio kutokea nikawaita ndugu na wazazi wangu waje kushuhudia kwa sababu lilikuwa la ajabu, siku ya Jumatatu nilijisikia vibaya nikaamua kwenda hospitali ya Wilaya Somanda kwa ajili ya vipimo,” alisema Regina.

“Nilifika hospitali nikawaeleza tukio zima, kisha nikafanyiwa kipimo cha mionzi na majibu ya kipimo hicho yalionyesha hapakuwa na kitu chochote tumboni,” alisema Regina.

Mwanamke huyo alisema kuwa baada ya kutoka hospitali waliendelea na maombi nyumbani hapo huku wakiwashirikisha viongozi wa dini na mnyama huyo alichomwa moto na viongozi wa dini.

Mama mzazi wa Regina Maimuna Fransic, alisema baada ya kupigiwa simu na mtoto wake alifika nyumbani hapo na kukiri kuwa alikuta amejifungua mnyama huyo na kubaki wanastaajabu.

“Kila mtu hapo ndani tulibaki tunashangaa hili jambo limetoka wapi, katika historia ya ukoo wetu halijawahi kutokea, mtoto wangu na mume wake wamekuwa wakiishi kwa kumtegemea Mungu,” alisema Maimuna.

Hata hivyo, alipoulizwa kama mtoto wake alikuwa na ugomvi na mtu, alisema kuwa hakuwahi kusikia jambo hilo au ndoa yake kuwahi kuingiliwa na mtu mwingine.

Naye Paul Manyangu mmoja wa majirani nyumbani hapo, alisema alishiriki kumsaidia mama huyo baada ya kupiga kelele chooni na kushangaa kuona amejifungua mnyama.

“Tulibaki kila mtu na mshangao na kuogopa sana, lakini ndiyo hali halisi iliyojitokeza kila kitu tunamwachia Mungu yeye ndiye anajua nini kipo nyuma ya pazia, lakini kwa jinsi ambavyo tumeishi na hii familia ni watu wa kumtegemea Mungu sana,” alisema Manyangu.

Daktari.

Mganga Mfadhiwi Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi (Somanda), Dk. Emmanuel Costanine, alikiri mama huyo kufika hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo ambavyo vilionyesha hakuwa na ujauzito wala hakujifungua.

Dk. Costantine alisema kuwa walimfanyia vipimo viwili, cha kwanza ni kipimo mkono ambacho kilionyesha hakuwa na ujauzito wowote na kipimo cha pili ni Ultrasound ambacho kilionyesha tumboni hakukuwa na kitu chochote na wala hakujifungua,” alisema Dk. Costantine.

Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, ACP Richard Abwao alikiri jeshi hilo kupokea taarifa za tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini ukweli wake ikiwamo kupata taarifa za kitaalamu kutoka kwa madaktari.