Baba amfuata mwana bungeni

17Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Baba amfuata mwana bungeni

RAIS John Magufuli jana alifanya uteuzi wa wabunge wawili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na balozi mmoja, mmoja kati yao akienda kukutana na mwanawe ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Alhaji Abdallah Bulembo akisalimiana na rais john magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, wabunge walioteuliwa ni Alhaji Abdallah Bulembo na Profesa wa Sheria Palamagamba Kabudi.

Bulembo ni baba wa Halima Bulembo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kagera kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Halima ndiye Mbunge mdogo kuliko wote katika Bunge la 11 alizaliwa miaka 25 iliyopita.

Bulembo, pia, ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi ya CCM.

Uteuzi wa wabunge hao umefanya idadi ya wabunge wote kufikia 391 ingawa nafasi moja inatarajiwa kuongezeka Jumapili katika uchaguzi mdogo wa jimbo Mbunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar.

Itakuwa ni mara ya pili kwa watu wenye uhusiano wa karibu kukutana bungeni baada ya marehemu Dk. Emmanuel Makaidi na mkewe Modesta kuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa wabunge wateule wataapishwa kwa taratibu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, "Rais Magufuli amemteua Benedicto Martin Mashiba kuwa Balozi. Kituo cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi Mteule Benedicto Martin Mashiba kitatangazwa baadaye," ilieleza zaidi taarifa hiyo.

Habari Kubwa