Baba watoto 3 jela miaka 30 kubaka binti darasa la 7

15Feb 2020
Daniel Limbe
Geita
Nipashe
Baba watoto 3 jela miaka 30 kubaka binti darasa la 7

MAHAKAMA ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela, Kabagambe Mihayo, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi wa darasa la saba.

Mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Buzirayombo wilayani Chato, alikamatwa na askari polisi Februali 10 na siku tatu baadaye, alifikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya ubakaji.

Katika kesi hiyo namba 45 ya mwaka 2020, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Semen Nzigo, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa alikuwa akimbaka mwanafunzi huyo (jina tunalo) kwa nyakati tofauti huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.

Alidai kitendo cha kushiriki ngono na mtu aliye chini ya miaka 18 ni kosa la jinai kwa mujibu wa Kifungu cha 130(1) na (2)(e) pamoja na Kifungu namba 131(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Mbele ya Mahakama hiyo, mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka ya ubakaji, alikiri kutenda kosa hilo huku akidai kuwa mtoto huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba kwenye Shule ya Msingi Buzirayombo ni mpenzi wake wa muda mrefu.

Sambamba na hilo, alisema uhusiano wao ni kama mke na mume licha ya kutambua kuwa mpenzi wake huyo ni mwanafunzi wa shule ya msingi.

Baada ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Alphonce Kagimbo, kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, alisema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshtakiwa analo kosa kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.

Kabla ya kutoa hukumu hiyo, mahakama hiyo ilitoa fursa kwa mshtakiwa kujitetea ili apunguziwe adhabu, ambapo alidai kuwa alifanya kitendo hicho kwa kupitiwa na shetani na kwamba ana mke na watoto watatu.

Hata hivyo, licha ya utetezi huo, mahakama hiyo ilimhukumu kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye kufanya ngono na watu walio na umri wa chini ya miaka 18.

Habari Kubwa