Babu wa kikombe afariki

30Jul 2021
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Babu wa kikombe afariki

MZEE maarufu wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, Ambilikile Mwasapila maarufu kwa jina la "Babu wa kikombe Loliondo"amefariki dunia.

Kwamujibu wa Mkuu wa wa Wilaya ya Ngorongoro, Mwalimu Raymond Mwangwala akizungumza na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu amesema Ambilikile alipelekwa kituo cha Afya cha Digodigo leo Julai 30,2021 majira  ya saa 9:45 alasiri kwa ajili ya matibabu.

Mwangwala, amesema ilipotimu saa 10:30 jioni mzee Ambilikile alifariki dunia na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Wasso wakati wakisubiri taratibu za mazishi kwa familia yake.

"Ni kweli amefariki dunia jioni ya leo na taratibu za mazishi zinafanyika na ndugu watakapokamilisha taratibu za mazishi tutawajulisha anazikwa wapi,"amesema

Mzee Mwasapila alijizolea umaarufu mkubwa pale alipogundua kikombe cha kuponya magonjwa mbalimbali na kupelekea watu kutoka maeneo mbalimbali kufika eneo la Digodigo (Samunge) kunywa kikombe hicho kwa gharama ya Sh.500

Pia aliwezesha barabara kutoka Kigongoni hadi Samunge kutengenezwa kwa kiwango cha changarawe ili kuwezesha wananchi kufika kunywa kikombe hicho ambacho watu mbalimbali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walifika kwa helkopta na msururu mkubwa wa magari kunywa kikombe hicho ambacho watu waliamini uponyaji.

Pia huduma za mitandao ya simu ambayo haikuwepo kijijini hapo ilipelekwa.