Bajeti  ijayo  trl.  32/-

14Mar 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bajeti  ijayo  trl.  32/-

BAJETI ya tatu ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha Sh. trilioni 32.476 kwa kipindi cha mwaka 2018/19.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akionesha mkoba wenye bajeti ya serikali mjini Dodoma ya mwaka 2017/18.

Akiwasilisha bungeni jana mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema mfumo wa bajeti ya mwaka huo umezingatia hali halisi ya upatikanaji wa mapato kutoka vyanzo mbalimbali.

Alisema mapato ya ndani, ikijumuisha ya Halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 20.89 sawa na asilimia 64 ya bajeti yote.

“Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh. trilioni 18 sawa na asilimia 13.6 ya pato la taifa. Mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia Sh. trilioni 2.15 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh. bilioni 735.6,” alisema Dk. Mpango.

Alitaja vyanzo vingine vya mapato kuwa ni pamoja na misaada na mikopo yenye masharti nafuu ya Sh. trilioni 2.67 kutoka kwa washirika wa maendeleo ikiwa ni asilimia nane ya bajeti yote.

Aidha, alisema serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 5.79 kutoka soko la ndani, ambapo Sh. trilioni 4.6 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva.

Pia alisema Sh. trilioni 1.19 ni mikopo mipya kwa ajili kugharamia miradi ya maendeleo ambazo ni sawa na asilimia 0.9 ya pato la taifa.

“Ili kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi muhimu ya miundombinu, serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 3.1 kutoka soko la nje,” alisema Dk. Mpango.

Akizungumzia upande wa matumizi, Waziri Mpango alisema kwa mwaka huu serikali inapanga kutumia Sh. trilioni 32.476, kati ya fedha hizo Sh. trilioni 20.468 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti.

Aidha, alisema matumizi ya kawaida yanajumuisha Sh. trilioni 10 kulipia deni la serikali, Sh. trilioni 7.369 mishahara, matumizi mengineyo (OC) Sh. trilioni 3.09, matumizi yatakayotokana na vyanzo vya ndani vya halmashauri Sh. bilioni 389.9.

MATUMIZI YA MAENDELEODk. Mpango alisema katika matumizi ya maendeleo, serikali itatumika Sh. trilioni 12.007, sawa na asilimia 37 ya bajeti na kwamba kiasi hicho kinajumuisha Sh. trilioni 9.876 sawa na asilimia 82.3 ambazo ni fedha za ndani na Sh. trilioni 2.130 sawa na asilimia 17.7 fedha za nje.

Alisema kiasi hicho, hata hivyo, hakihusishi uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya umma na ubia kati ya uwekezaji wa moja kwa moja wa sekta binafsi, mashirika ya umma na ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumzia kuhusu miradi kielelezo itakayopewa msukumo, Waziri Mpango alitaja ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Standard Gauge kiasi cha Sh. trilioni 1.4 ambazo ni fedha za ndani.

Katika mwaka 2018/19, Dk.Mpango alisema kiasi cha Sh. bilioni 495.6 zimetengwa kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege ya pili aina ya Dreamliner-Boeing 787, ununuzi wa ndege moja mpya aina ya Bombadier Dash 8 Q400 na kuanza uendeshaji wa ndege mpya Boeing 787 na Bombardier CS 300.

Alisema katika mwaka huo, Sh. bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa na ujenzi wa njia kuu za kupitishia maji katika mradi wa Stieglers' Gorge.

Habari Kubwa