BAJETI 2019/20 Yabana, yapuliza

14Jun 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
BAJETI 2019/20 Yabana, yapuliza

NI shangwe na kilio. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na makadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha kuwa na mambo mengi yanayofurahisha na machache kuumiza.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

Makadirio hayo ya kukusanya na kutumia Sh. trilioni 33.11, yaliwasilishwa bungeni jijini Dodoma jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Katika hotuba yake, Dk. Mpango aliibua shangwe bungeni alieleza kuwa anapendekeza kufuta baadhi ya tozo zinazolalamikiwa kuwa kero katika biashara na uwekezaji.

Dk. Mpango mbali na kupendekeza kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika baadhi ya bidhaa, aliibua shangwe alipotangaza kuwa serikali inakusudia kufuta tozo 54 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kibiashara na uwekezaji nchini.Tozo hizo 54 ni zinazotozwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.Hata hivyo, mtaalamu huyo wa uchumi aliibua minong'ono alipoeleza mapendekezo machache ambayo yalionekana kutowafurahisha watunga sheria hao.Katika mapendekezo yake, Dk. Mpango aliibua shangwe alipoeleza kuwa serikali inakusudia kufuta tozo mbalimbali zikiwamo zilizolalamikiwa na wafanyabiashara waliokutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 7, mwaka huu.Tozo na ada zinazopendekezwa kuongezwa na kuonekana kutowafurahisha wabunge, ni pamoja na ongezeko la ada ya usajili wa magari kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 50,000, ongezeko la ada ya leseni ya udereva kutoka Sh. 40,000 hadi Sh. 70,000, kurejeshwa kwa VAT katika taulo za kike na tozo ya nywele za bandia zinazozalishwa nchini na kuagizwa nje.SURA YA BAJETIDk. Mpango alisema kwa kuzingatia shabaha, malengo na Sera za Bajeti kwa Mwaka 2019/20, sura ya bajeti inaonyesha kuwa, jumla ya Sh. trilioni 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.Alibainisha kuwa jumla ya mapato ya ndani yanarajiwa kuwa Sh. trilioni 23.05, sawa na asilimia 69.6 ya bajeti yote.Waziri huyo alisema kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya Sh. trilioni 19.1, sawa na asilimia 12.9 ya Pato la Taifa.Alisema mapato yasiyo ya kodi kwa mwaka 2019/20 yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 3.18 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh. bilioni 765.5.Dk. Mpango pia alisema serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 4.96 kutoka soko la ndani. Kati yake, Sh. trilioni 3.46 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva na kiasi cha Sh. bilioni 1.5 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo."Kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 2.32 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara," alisema.Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. trilioni 2.78 ambayo ni asilimia nane ya bajeti."Misaada na mikopo hii inajumuisha miradi ya maendeleo Sh. trilioni 2.31, mifuko ya pamoja ya kisekta Sh. bilioni 199.5 na misaada na mikopo nafuu ya kibajeti Sh. bilioni 272.8," alisema.MATUMIZIDk. Mpango alisema serikali inapanga kutumia Sh. trilioni 33.11 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo.Alisema kuwa Sh. trilioni 20.86 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha Sh. trilioni 9.72 kwa ajili ya ulipaji wa Deni la Serikali na Sh. trilioni 7.56 kwa ajili ya mishahara.Alisema Sh. trilioni 3.58 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo ikijumuisha Sh. bilioni 460.5 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya halmashauri.Alibainisha kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020."Matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 12.25 sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ambao kiasi cha Sh. trilioni 9.74 ni fedha za ndani na Sh. trilioni 2.51 ni fedha za nje," alisema.Alisema kiasi cha Sh. trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha reli ya kati ya kisasa (SGR), Sh. trilioni 1.44 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji, maarufu Stiegler's Gorge na Sh. bilioni 450 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu."Na Sh. bilioni 288 ni kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, serikali imetenga jumla ya Sh. bilioni 600 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme," alisema.

 

 Imeandikwa na Augusta Njoji na Sanula Athanas, DODOMA

Habari Kubwa