Bajeti Kilimo yamkuna Mbunge Ditopile

18May 2022
Mary Geofrey
Nipashe
Bajeti Kilimo yamkuna Mbunge Ditopile

MBUNGE wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Ditopile, ameimpongeza serikali kwa kutenga bajeti ya kilimo anayoamini inakwenda kufanya mapinduzi kwenye sekta hiyo.

MBUNGE wa Viti Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Ditopile.

Ditopile amesema hayo leo, bungeni jijini Dodoma wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2022/23 ya Sh. bilioni 751.12 ikiwa imeongezeka kutoka Sh. bilioni 294.16 ya bajeti iliyopita.

Bajeti hiyo iliwasilishwa jana Jumanne na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na kusema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 155.34 ikiwa sehemu kubwa ya fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na miundombinu ya uhifadhi wa mazao.

Alisema pia kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao, kuimarisha utafiti wa kilimo, uzalishaji wa mbegu na utoaji wa ruzuku.

Akichangia bajeti hiyo, Ditopile amesema, kwa kipindi kirefu bajeti ya kilimo imekuwa ikilalamikiwa na wabunge kwamba ni kidogo lakini mwaka huu imepanda huku akimpongeza Rais Samia kwa kuwateua Bashe kuwa waziri na Anthony Mavumbe kuwa naibu ambao wanaonyesha mwanga kwenye sekta hiyo.

"Nimpe pongezi Rais Samia Suluhu Hassan, kwa hakika ameonyesha yeye ni mkulima mwenzetu na anajali kwa vitendo maslahi ya wakulima nchini na hilo amedhihirisha kwa kutuletea waziri na naibu wake wenye kujali wakulima,” amesema Ditopile

Ameongeza kusema kuwa, “Kilimo kinafanyika sana nchini, ndio maana katika takwimu za serikali tunaelezwa kilimo kimeajiri asilimia kubwa ya Watanzania, lakini cha kushangaza mkulima anakutana na serikali baada ya kuvuna.”

Amesema kilimo ni utafiti na utaalamu, ni udongo ama mbegu ni sayansi na teknolojia, ni dawa, ni maji kwa maana ya mvua au umwagiliaji, ni miundombinu ya uvunaji, ni urutubisho, ni uhifadhi na ni soko na ukikosoea jambo moja umeondoa tija kwenye kilimo.

Mbunge huyo amesema, “Tusiache sayansi na teknolojia, twende sawa na dunia, kwa nini tunakataa mbegu za GMO, tunazikataa kwa nini, tunalima Pamba tunataka kuzalisha nguo, lakini Brazili, India na China wanatumia GMO, sisi tunachokitaka tuleteeni na mkulima aamue, mnasema zina madhara ni uongo mtupu,”amesisitiza.

Aidha, Ditopile amezishauri Wizara ya Kilimo kufanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kuwezesha kuwasaidia wakulima kulima mazao yenye tija kwa kipindi fulani.

“Nishauri kwamba, tuanzie sokoni, leo hii uhaba wa mafuta ya kula umekuja kujulikana kupitia viwanda vya kibiashara. Niombe wizara ya kilimo na ya biashara mkae pamoja na kushirikiana ili kuwashauri wakulima walime mazao gani yenye tija kwa musimu husika,” amesema Ditopile na kuongeza:

“Bajeti ya kilimo imepanda, niliwahi kushauri vijana lazima watengenezewe namna ya kushiriki kwenye kilimo, naona kundi kubwa hili ambalo nimekuwa mtetezi wao mmewakumbuka na mnakwenda kutoa vitendea kazi na watashiriki sasa kwenye kilimo.”

Habari Kubwa