Bajeti ya kwanza ya Samia leo

10Jun 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bajeti ya kwanza ya Samia leo

MACHO na masikio ya Watanzania yanatarajiwa kuelekezwa bungeni jijini Dodoma leo, wakati Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22 itakapowasilishwa ili ijadiliwe na kupitishwa na chombo hicho.

Rais Samia Suluhu Hassan.

Tanzania na nchi zingine za Afrika Mashariki zinatarajiwa kuanika bajeti zake, Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba akitarajiwa kuwasilisha bajeti ya Sh. trilioni 36.3, sawa na ongezeko la asilimia nne kulinganishwa na bajeti ya mwaka huu.

Bajeti inayowasilishwa leo ni ya kwanza chini ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyechukua uongozi wa nchi Machi 19, mwaka huu kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Magufuli.

Mapendekezo yaliyotolewa kwenye ukomo wa bajeti, yalibainisha kuwa kati ya fedha hizo, asilimia asilimia 37 ya bajeti yote itaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi maendeleo.

Katika mapendekezo hayo ya awali, serikali inatarajiwa kutumia Sh. trilioni 10.7 (asilimia 29.5 ya bajeti yote) kulipa fedha madeni.

Miongoni mwa vipaumbele vya serikali vilivyotajwa kwenye mapendekezo ya awali ni kugharamia miradi ya kipaumbele na kimkakati, Deni la Serikali, mishahara ya watumishi, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, mpango wa elimu msingi bila ada na uendeshaji wa ofisi.

Katika mapendekezo yaliyotolewa kwenye wizara mbalimbali za kisekta, serikali inalenga kuipa sekta binafsi uzito mkubwa huku ikipendekeza utekelezaji wa miradi ya kielelezo ikiwamo ya Kufua Umeme wa Maji - Julius Nyerere MW 2,115, kuboresha Shirika la Ndege (ATCL) na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa.

Miradi mingine ya kielelezo ni pamoja na wa makaa ya mawe, Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga.

Pia bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) na mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) mkoani Lindi.

MAONI YA WABUNGE

Wakati Watanzania wakisubiri bajeti hiyo, wabunge wamebainisha matarajio yao, wakisema itajikita kwenye utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu, alisema matarajio ni kuona vipaumbele ambavyo walikuwa wakivisema katika ilani hasa kwenye sekta za barabara, maji, miundombinu ya elimu, afya na masuala mazima ya kilimo na ujasiriamali yakitekelezwa kwa kiwango cha juu.

Mbunge wa Bukene (CCM), Selemani Zedi, alisema  matarajio yake kwenye  bajeti ni kuona serikali inaainisha vyanzo vipya vya mapato.

Mbunge wa Viti Maalum, Anastazia Wambura, alisema masuala ya maji yatapata majibu kwenye bajeti hiyo.

Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi, alisema anatamani kuona kiu ya wananchi ikienda kutimizwa katika maeneo ya barabara.

Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu, alisema anatazamia bajeti iende ikawaguse wananchi wa hali ya chini.

"Lakini pia sasa hizi tuna changamoto ya ajira kwa vijana, hivyo miradi ya uwekezaji ambayo imetengewa fedha kama itapelekwa basi itatoa mwanya wa miradi kuendelea na kutengeneza ajira kwa vijana,” alisema.

Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest, alisema anatarajia kuona bajeti inayogusa watu na siyo bajeti ya vitu kwa kuwa kwa muda mrefu kumekuwapo na bajeti zinaohusu vitu na fedha nyingi kupelekwa kwenye wizara ambazo hazigusi moja kwa moja watu.

Habari Kubwa