Bajeti yapongezwa kila kona

15Jun 2019
Gwamaka Alipipi
DAR
Nipashe
Bajeti yapongezwa kila kona

SIKU moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuwasilisha bungeni bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha, wasomi, wananchi na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na kijamii, wameisifu wakisema imegusa jamii kubwa ya Watanzania.

Dk. Mpango juzi aliwasilisha mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/2020 yenye thamani ya Sh. trilioni 33.11, huku akitaja vipaumbele vya serikali kuwa ni kuendeleza viwanda na kilimo, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote.

Vingine ni kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli, bandari, nishati, barabara, madaraja, na viwanja vya ndege na upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, ujuzi, chakula na lishe bora, huduma za majisafi na salama.

Mhadhiri kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Stephen Kirama, alisema ni bajeti yenye mambo mengi na yanayotia matumaini kwenye sekta zote muhimu kama vile kilimo, miundombinu na biashara.

Alisema licha ya bajeti hiyo kugusa sehemu kubwa ya jamii ya Watanzania,  haijamgusa mtu mmoja mmoja, akitolea mfano makato ya kodi ya mshahara (PAYE) ambayo hayajafanyiwa marekebisho.

"Bajeti imegusa sekta za ujumla, kodi za biashara kwani wafanyabiashara wameshushiwa neema, lakini PAYE ambayo inagusa idadi kubwa ya wananchi nayo ingepewa kipaumbele," alisema.

Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), alisema ni bajeti nzuri iliyojaa matumaini kwa Watanzania wengi.

Prof. Semboja alisema bajeti ya mwaka 2019/20 ni tofauti na bejeti zilizopita kwa kuwa imeeleza inakwenda kutekeleza masuala ambayo yanawagusa kundi kubwa la Watanzania.

"Kupunguzwa kwa kodi nyingi kwa wafanyabiashara imedhihirisha kuwa serikali imekuwa ikisikiliza maoni ya sekta binafsi, imefuta na kurekebisha mifumo ya kodi ambayo ilikuwa ni kandamizi," alisema Prof. Semboja.

Hata hivyo, Prof. Semboja alitoa angalizo kwa serikali akiitaka kutotegemea vyanzo vya kodi peke yake katika kuendesha mambo yake, bali iangalie vyanzo vingine.

Rais wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta), Tumaini Nyamuhokya, alisema licha ya kuwa ni bajeti ambayo imegusa kundi kubwa la wafanyabiashara, imemsahau mfanyakazi.

"Sisi kwetu bado ni pigo. Tunawaomba wabunge watusaidie, kama wameona kuwakumbuka  wafanyabiashara walipaswa kuwakumbuka na wafanyakazi ambao ndio wengi," alisema Nyamhokya.

Alisema licha ya kodi nyingi kupunguzwa, bajeti hiyo imesahau kupunguza PAYE ambayo imekuwa ikipigiwa kelele miaka mingi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Tony Swai, alisema bajeti imegusa maeneo mengi mazuri, lakini utaratibu wa kuondoa mawakala wa forodha hautakuwa jambo jema.

Alisema mawakala wa forodha wanatambulika na Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ya Afrika Mashariki ya mwaka 2009 kifungu cha 145 (1) (2) pamoja na kifungu cha 146.

Swai alisema kuondolewa kwa mawakala hao kunaweza kusababisha zaidi ya watu  10,000 kupoteza ajira.

Habari Kubwa