Bakwata yatoa siku 30 kusajiliwa ndoa

20Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
MOSHI
Nipashe
Bakwata yatoa siku 30 kusajiliwa ndoa

BARAZA Kuu la Waislamu Mkoa wa Kilimanjaro (Bakwata), limetoa siku 30 kwa viongozi wake wa madrasa, misikiti na waliopewa dhamana ya kufungisha ndoa kwa mujibu wa sheria, kutekeleza agizo la Mufti wa Tanzania, Shekhe Abubakar Zuberi aliyetaka wasajiliwe.

Muda huo maalum wa kutekeleza agizo hilo, ulitangazwa jana na Katibu wa Bakwata mkoani hapa, Awadh Lema, wakati akizungumza na viongozi mbali mbali wa misikiti wakiwamo maimamu wa mkoa huo.

Aprili 13, mwaka huu, Bakwata, ilizindua mpango mpya wa vyeti vya ndoa, usajili wa madrasa na walimu, misikiti na utoaji wa vitambulisho kwa wafungishaji ndoa katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Al-Haramain, iliyopo Kariakoo, Ilala, jijini Dar es Salaam.

"Nimetoa siku 30 kwa Mkoa wa Kilimanjaro ili wahusika waweze kujisajili kulingana na maelekezo ya Mufti na endapo mtu hatajisajili, Bakwata itashindwa kumtambua na atakuwa siyo mtu sahihi kutekeleza majukumu hayo,'' alisema Lema.

Alisema kusajiliwa kwa misikiti na madrasa kutasaidia kuyaweka mambo wazi pamoja na kuhifadhi kumbukumbu zao katika ofisi za baraza hilo katika ngazi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Lema, kuna umuhimu mkubwa kwa madrasa na misikiti yote kujulikana na kwamba utambulisho huo utaisaidia Bakwata kusaidiwa katika mambo mbalimbali.

Hata hivyo, Kaimu Shekhe wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, wakati anazungumza na viongozi hao kuhusu vyeti vya ndoa, aliwataka wote wenye vitabu vya ndoa vya zamani kuviwasilisha ofisini kwake mara moja na kuchukua vipya.

Kutokana na utekelezaji wa agizo hilo, Imamu wa Kijiji cha Sanya Juu, Wilaya ya Siha, Hamza Shekhe na Mwenyekiti wa Bakwata Wilaya ya Hai, Omari Maamud kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa mpango huo ni mzuri na utasaidia kufahamu mambo mbalimbali yanayofanyika katika madrasa zao na misikiti yao.

Habari Kubwa