Balaa dawa ‘kasongo mundende’ kwa nguvu za kiume

16Jul 2017
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Balaa dawa ‘kasongo mundende’ kwa nguvu za kiume

JE, umewahi kusikia jina la kasongo mundende, vumbi la Kongo, kizizi cha mkuyati na majina mengine aina hiyo yanayowakilisha dawa za kienyeji, zinazouzwa maeneo mbalimbali jijini kwa nia ya kuongeza nguvu za kiume?

Kama ndivyo, inaelezwa kuwa dawa aina hiyo zinaweza kuwa hatarishi kwa afya ya watu badala ya kuwa tiba kwao endapo zitatumika ovyo pasi na kujua viambata vyake na kiwango kilichomo kabla ya kutumiwa kwake.

Kasongo mundende (jina linalotajwa kuwa ni la Kikongo) na dawa nyingine za kienyeji zenye majina mbalimbali, zimekuwa maarufu katika maeneo ya mijini, ikiwamo jijini Dar es Salaam, ambako baadhi ya vijana huungana na wanaume walio na matatizo katika masuala ya uzazi kujiongezea nguvu – ikielezwa kuwa huwasaidia watumiaji kuwarejeshea ‘ungangari’ wao kama ilivyo kwa dawa rasmi za jamii ya ‘viagra’.

Katika uchunguzi wake, Nipashe iliwahi kubaini kuwa vijana wanaochangamkia zaidi matumizi ya dawa hizo ni wale ambao hupewa kazi maalumu na wapenzi wao wenye umri mkubwa kwa nia ya kuwaridhisha na mwishowe kuambulia zawadi nono ya fedha na vitu vya thamani.

Ilielezwa kuwa baadhi ya dawa hizo, licha ya kuweza kuwasaidia watumiaji kwa muda mfupi, zinaweza kuwaweka katika balaa kubwa la kuua kabisa nguvu zao asilia za kiume; kuwasababishia upofu baadaye, kuwaletea maradhi ya figo na pia kuwasababishia kiharusi na shinikizo la damu.

Baadhi ya dawa hizo huingizwa nchini kutoka katika nchi jirani ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mara nyingi huingizwa nchini na madereva na watu wa malori yanayosafiri kati ya Tanzania na nchi hizo.

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki kuhusiana na kuendelea kushamiri kwa matumizi ya dawa asili za kuongeza nguvu kwa wanaume, Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Paulo Mhame, alisema ni kweli kuna idadi kubwa ya wanaume wanaokimbilia kutumia dawa aina hiyo kwa nia ya kupata nafuu ya matatizo yanayowakabili, lakini changamoto kubwa inayoweza kuwaletea shida wengi wao ni kujua kama kweli zina matokeo chanya yasiyokuwa na madhara makubwa ya kiafya.

Mhame alisema ni kweli kwamba ipo mimea ambayo hutumiwa kutengeneza dawa sahihi za matatizo hayo, lakini nayo inaweza kuwa na madhara makubwa inapotumiwa holela na bila ushauri wa kitaalamu.

Alisema baadhi ya watu hutumia shida za wenzao kwa nia ya kujiingizia fedha bila kujali madhara yanayoweza kutokea na kwamba hilo, linapaswa kuzingatiwa na watumiaji wa dawa hizo.

Hata hivyo, Mhame alisema kuwa hadi sasa hakuna takwimu zinazoonyesha idadi ya watu walioathirika kutokana na matumizi holela ya dawa hizo, ambazo baadhi miti yake hupatikana katika hifadhi mbalimbali za misitu nchini ikiwamo maeneo ya hifadhi ya Selous.

Habari Kubwa