Balozi aipongeza OSHA usimamizi sheria ya usalama na afya kazini

08Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Balozi aipongeza OSHA usimamizi sheria ya usalama na afya kazini

BALOZI wa Heshima wa Seychelles nchini, Maryvonne Pool, ameipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikia katika usimamizi wa sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi yenye lengo la kulinda nguvu kazi ya Taifa.

Balozi wa Heshima wa Seychelles hapa nchini, Maryvonne Pool,
akizungumza na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipotembelea ofisi za OSHA kwa ajili ya kusajili sehemu yake ya kazi na kujifunza namna ambavyo OSHA inafanya kazi.

Aidha Balozi Pool, amesema anatambua kazi nzuri  inayofanywa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na kupitia sheria hiyo maeneo mengi ya kazi yanatambulika na kuzingatia viwango vya usalama na afya kazini.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini Dar es salaam wakati alipotembelea ofisi za OSHA kwa lengo kufanya usajili wa moja ya miradi ambayo ofisi yake ni mbia pamoja na kujifunza namna ambavyo taasisi hiyo inavyotekeleza.

 “Naipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa na taasisi muhimu kama hii ambayo inasaidia kulinda nguvu kazi ya nchi na kimsingi nimekuwa nikiwasikia sana siku hizi na nafahamu jinsi mlivyojipanga katika kutekeleza majukumu yenu ya msingi,” amesema Balozi Pool.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda akimsikiliza Balozi wa Heshima wa Seychelles hapa nchini, Maryvonne Pool (hayupo pichani) alipotembelea ofisi za OSHA.

Akiwa katika ofisi hizo ameahidi kushirikiana na OSHA katika kuviwezesha vikundi vya wakulima wadogo wanaofanya shughuli zao katika wilaya za pembezoni mwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kuhakikisha vikundi hivyo vinasajiliwa na OSHA kwa ajili ya kujikinga na madhara yatokanayo na shughuli za kilimo.

“Sisi tunafanya miradi mbali mbali ya kuwawezesha wakulima kuboresha uzalishaji na kupata masoko ya mazao ya kilimo na japokuwa tumekuwa tukiwawezesha wakulima kupata vifaa muhimu vya kujikinga kama vile viatu vya shambani (Gunboots) lakini tunaona ipo haja ya kuwahamasisha wakulima kuwa katika vikundi vya uzalishaji na kuwawezesha kupata usajili wa OSHA ili muendelee kuwaongoza kufanya kazi zao kwa usalama zaidi,” amesema Balozi Pool.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake imefarijika kutambua kwamba juhudi za serikali za kulinda nguvukazi ya Taifa zinaonekana.

“Tumefurahi sana leo kutembelewa na Balozi wa Heshima wa Seychelles hapa nchini kwetu ambaye amekuja kusajili eneo lake la kazi. Tumepata fursa ya kushirikishina mambo mengi na kubadilishana uzoefu jinsi ambavyo nchi zetu zinasimamia masuala ya afya na usalama ambapo amefurahi sana kuona kwamba nchi yetu ina mfumo madhubuti wa kusimamia usalama na afya ili kulinda nguvu kazi ya Taifa,” amesema  Mwenda. 

Katika ziara hiyo Balozi Pool amefanikiwa kusajili mradi ambao ofisi yake ni mbia na kupatiwa cheti cha usajili papo hapo. Aidha, amepata fursa ya kubadilishana uzoefu na Mtendaji Mkuu wa OSHA kuhusu mifumo ya usimamizi wa masuala ya Usalama na Afya baina ya Tanzania na Visiwa vya Seychelles ambapo alieleza kuwa nchi yake ina sheria kali zinazohusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Habari Kubwa