Balozi akanusha vikwazo Tanzania

21Nov 2020
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Balozi akanusha vikwazo Tanzania

BALOZI wa Tanzania nchini Ubelgiji na Mwakilishi katika Umoja wa Ulaya, Jestas Nyamanga, amekanusha taarifa kuwa Bunge la Ulaya limeiwekea vikwazo vya kiuchumi Tanzania na kuifungia mikopo na misaada.

Kutokana na ufafanuzi huo, Balozi nyamanga amewataka Watanzania kupuuza taarifa hizo, alizoziita kuwa ni za upotoshaji.

Taarifa zilizotolewa hivi karibuni zilisema Tanzania kutokana na vikwazo hivyo, itakosa Sh. tilioni 1.6.

Katika video iliyorushwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii na kuonyeshwa mara kwa mara kwenye kituo cha Luninga ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Balozi Nyamanga  anabainisha kuwa hakukuwa na kikao cha bunge bali kamati ya mambo ya nje ya bunge hilo.

“ Leo (juzi) tarehe 19 asubuhi hapa Ubelgiji, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya, ilikutana katika kikao chake cha kawaida.  Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika kamati hiyo ilihusu Tanzania na hali ilivyo baada ya uchaguzi mkuu kukamilika.

“Huu ni utaratibu wa kawaida kabisa kujadili na kuweka majadiliano kuhusu mbia wao mkuwa wa maendeleo pindi tu uchaguzi unapokuwa umekamilika na hasa uchaguzi mkuu, “ alisema.   

Balozi Nyamanga alisema taarifa ya kuwa Bunge la Ulaya limeazimia kuiwekea Tanzania vikwazo ni upotoshaji unaozushwa na watu wasioitakia nchi mema.

“Taarifa hizi ni za uongo hazina ukweli wowote. Kikao hicho cha kamati ya bunge hakikutoa azimio lolote kuhusu Tanzania. Kilichofanyika ni kuwapa wabunge kutoa mawazo yao kuhusu hali ya Tanzania baada ya uchaguzi,” alisisitiza.

 Alibainisha kuwa kikao ni cha Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Umoja wa Ulaya yenye wabunge 71 na si bunge zima na kwamba wabunge katika vikao vyao kila mmoja ana haki ya kutoa mawazo yake.

Balozi Nyamanga alisema Bunge la Ulaya  lina wabunge 705 na kama ilivyo Tanzania, wabunge wana haki ya kutoa mawazo yao, hivyo katika kikao hicho, wabunge hao watao walitoa mawazo tofauti tofauti wanavyoona lakini hakuna azimio lililotolewa.  

“Si kweli kuwa fedha hizo zimesitishwa, utekelezaji wa miradi mbalimbali unaendelea tena vizuri na hakuna zuio lolote la kusitisha fedha hizo,” alisema.  

Alisema pia hakuna mjadala  wowote unaoendelea kwenye Bunge la Ulaya kuhusu kuiwekea Tanzania vikwanzo ikiwamo kuuza bidhaa zake katika nchi hizo.  

Nyamanga aliwahakikishia wananchi kuwa uhusinao wa Tanzania na umoja wa nchi hizo ni mzuri kwa zaidi ya miaka 45 iliyopita na kwamba tangu mwaka 1975 kumekuwa na ushirikiano mzuri wa maendeleo baina ya pande hizo mbili.

Habari Kubwa