Balozi mpya DRC aahidi kushirikiana na Magufuli

24Feb 2016
Beatrice Shayo
Dar
Nipashe
Balozi mpya DRC aahidi kushirikiana na Magufuli
  • “Tutakaa kwa pamoja na Rais kuangalia ni njia gani za kuwasaidia wafanyabiashara hawa ili kuwaondolea vikwazo katika biashara.”
  • Wakati mwingine, kontena linaweza kufika mapema, lakini unatakiwa kulipia gharama za kuchelewesha. Bado tuna tatizo, wanatupatia muda mchache wa kurudisha kontena bila kujali vikwazo tunavyokutana navyo barabarani.

BALOZI mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapa nchini, Jean Mutamba, ameahidi kushirikiana na Rais Dk. John Magufuli, (pichani), kutatua vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wafanyabiashara ili nchi zote mbili zinufaike kiuchumi.

Balozi mpya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) hapa nchini, Jean Mutamba.

Alitoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati wa halfa ya kumkabirisha.

Hafla hiyo iliyoambatana na maombi ya kumuombea balozi huyo afanye kazi zake kwa umakini, pia ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara wa DRC.

Balozi Mutamba alisema amejulishwa kuwapo kwa vikwazo mbalimbali kwa wafanyabiashara wa nchini Kongo, jambo ambalo atalishughulikia kwa kushirikiana na Rais Magufuli.

Hata hivyo, alisema matatizo yaliyosemwa na wafanyabiashara wa Kongo watayachunguza kwa kina na kuona ni jinsi gani ya kuwasaidia ili wasifanye kazi zao katika mazingira magumu.

“Tutakaa kwa pamoja na Rais kuangalia ni njia gani za kuwasaidia wafanyabiashara hawa ili kuwaondolea vikwazo katika biashara,” alisema Balozi Mutamba.

Alisema lengo la kutatua changamoto hizo ni kuhakikisha nchi hizo mbili zinakua kiuchumi pamoja na kuwapo kwa ushindani wa kibiashara.

Pia alisema atawasilisha changamoto ya kupatikana kwa kibali cha kusafiri ambayo inawakabili wafanyabiashara wa Kongo ili Rais Magufuli aone namna ya kuitatua.

Aidha, alisema ataendelea kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Kongo huku akiahidi kufanya kazi kwa kasi kama ya Rais Magufuli.

Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kongo waishio Tanzania, Mukendi Kabobu, alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutakiwa kulipia gharama za kontena linapocheleweshwa kurudishwa licha ya kukutana na vikwazo barabarani.

“Wakati mwingine, kontena linaweza kufika mapema, lakini unatakiwa kulipia gharama za kuchelewesha. Bado tuna tatizo, wanatupatia muda mchache wa kurudisha kontena bila kujali vikwazo tunavyokutana navyo barabarani,” alisema
Kabobu.

Alimuomba balozi huyo kuwaombea kwa Rais wa Kongo, Joseph Kabila, kuwajengea bandari yao nchini Tanzania ili iwarahisishie utendaji wa kazi zao.

Mwakilishi wa Jumuiya ya Wakongo waishio Tanzania (CCT), Mafimbo Madwari, alisema nchi za jirani zisiwe na vibali vya kusafiri kwa sababu mwingiliano wa Tanzania na Kongo ni mkubwa na una manufaa katika uchumi wa nchi.

Alisema gharama za kupata kibali cha kusafiri ni kubwa, hivyo wameomba kupunguziwa ili waishi kwa usalama.

Aidha, jumuiya hiyo imempongeza Rais Magufuli kwa utendaji wake wa kazi na kuahidi kushirikiana kwa pamoja katika kuongeza uchumi wa nchi.