Balozi Mulamula afanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia

07Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Balozi Mulamula afanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Dk. Taufila Nyamadzabo, kuhusu masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Juni 7, katika Ofisi ya Waziri Mulamula jijini Dodoma, ambapo Waziri huyo amesema mahusiano hayo yamelenga kunufaisha miradi ya maendeleo nchini.

Akiongelea uhusiano baina ya Tanzania na Benki ya Dunia Balozi Mulamula amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha mahusiano kati ya Tanzania na Benki hiyo yanaimarika na kuendeleza uwezo wa Watanzania wanaosimamia miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki ya Dunia ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta binafsi na kuifanya kuwa imara.

“leo hapa tumejadiliana juu ya mahusiano yetu, kuangalia namna ya kuyaboresha ili kunufaika na miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo, kuwajengea uwezo watu wetu wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo na uimarishaji wa Sekta binafsi ili kuwa imara na hivyo kufikia maendeleo ya kweli,” amesema Balozi Mulamula.

Akiongelea kuhusu mipango ya Serikali ya kuimarisha Sekta Binafsi Mhe Waziri Mulamula amemuhakikishia Dkt. Taufilo nia na mtizamo wa Serikali wa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuwekeza nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi hasa ikizingatiwa kuwa Benki ya Dunia inachukulia sekta binafsi kama chachu ya maendeleo na hivyo kuwa na miradi ya kusaidia ukuzaji wa Sekta binafsi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji huyowa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika kundi la kwanza Dkt. Taufila Nyamadzabo amesema miongoi mwa mambo waliyojadili leo ni pamoja na umuhimu wa kuhusisha sekta binafsi na kuiendeleza.

Habari Kubwa