Balozi Seif: Kiwango cha elimu kimeshuka Zanzibar

29Feb 2016
Mwinyi Sadallah
Nipashe
Balozi Seif: Kiwango cha elimu kimeshuka Zanzibar

MAKAMU Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, amesema nguvu za pamoja ndio msingi wa kukabili matatizo ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu, ukosefu wa ajira kwa vijana na unyanyasaji mkoa wa Kaskazini Unguja.

MAKAMU Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi

Ushauri huo aliutoa jana alipokuwa akiizindua Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja (JMMK) katika hafla iliyofanyika Malindi, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema takwimu zinaonyesha wazi kwamba mkoa wa Kaskazini Unguja unaongoza kwa kushuka kwa kiwango cha elimu na kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji, uchafuzi wa mazingira na mpasuko wa umoja unaosababishwa na tofauti za kidini na kisiasa ambazo zimesababisha kudidimia kwa hadhi na heshima ya mkoa huo.

“ Mkoa wetu hivi sasa umevamiwa na watu ambao wanatumia dini na siasa kwa lengo la kuwagawa wananchi, mambo ambayo kama hawakuwa makini watu hao wanaweza kuwaweka mahali pabaya wananchi wake,” alionya.

Alisema kipindi kirefu sasa shule za mkoa wa Kaskazini Unguja hazifanyi vizuri katika mitihani ya kitaifa, hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya mkoa.

Balozi Seif aliitaka JMMK kujipanga vizuri kimpango na kimkakati kwa upande ili kukuza kiwango cha elimu na hatimaye mkoa kurejesha hadhi yake.

Alisema ili malengo hayo yafanikiwe vyema, jumuiya hiyo inahitaji kuwa na ushirikiano wa karibu na viongozi wa shule zote zilizoko ndani ya mkoa, wazazi, taasisi za kijamii na wanafunzi wenyewe.

kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir, alisema nui muhimu kwa wana jumuiya kujitolea nguvu zao ili kufikia malengo kwa wakati muafaka.

Akizitaja changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mkoa huo kupotea kwa mila , silka na utamaduni ndani ya jamii na kuwa chimbuko la kubuniwa kwa jumuiya hiyo ya Maendeleo ya Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unaguja.

Wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Jumuiya hiyo Rais Mstaafu Dk Salmin Amour Juma, Balozi Seif Ali Iddi, Fatma Bakari Mohamed, Ali Ameir Mohammed na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye ni mjumbe wa heshima.
0000

Habari Kubwa