Balozi Wright amuenzi mwanaharakati Martin Luther King

18Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Balozi Wright amuenzi mwanaharakati Martin Luther King

MAREKANI leo inaadhimisha sikukuu ya kitaifa ya kumbukumbu ya kuenzi maisha ya urithi wa kinara mpigania haki za kiraia, mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel na mwanaharakati wa haki, usawa na utu wa mwanadamu, Martin Luther King, Jr.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, katika kuadhimisha siku hiyo, amesema watu duniani kote wanaifahamu hotuba mashuhuri ya “Nina ndoto” (I have a dream) aliyoitoa Martin Luther King mwaka 1963, akizungumzia matumaini yake ya watu wa rangi zote kuishi kwa amani na utangamano.

Balozi Wright katika salamu zake kupitia vyombo vya habari jana, alisema kiini cha hotuba hiyo iliyobeba ujumbe mzito kilikuwa ni tofauti kubwa iliyokuwapo kati ya ndoto aliyokuwa nayo Dk. King na hali halisi ya ubaguzi wa rangi iliyokuwapo nchini Marekani wakati huo.

“Kwa masikitiko makubwa, Dk. King aliuawa kabla ya kushuhudia ndoto yake ikitimia. Ni wazi kuwa hadi hivi leo, bado Marekani inahangaika ikikabiliwa na athari za muda mrefu za mifumo ya ubaguzi wa rangi, kama ambavyo dunia imeshuhudia katika tukio la mauaji ya George Floyd, mwaka jana,” alisema.

Balozi Wright alisema Taifa la Marekani limejengwa katika imani kwamba binadamu wote waliumbwa wakiwa sawa na wana haki za kimsingi za binadamu ambazo hawawezi kutenganishwa nazo.

Alisema katika maisha na kazi zake, Dk. King aliipa changamoto Marekani na kuitaka iishi kwa mujibu wa ahadi na maadili ya kimsingi ambazo taifa hilo limejengwa.

“Harakati hizi ni kitovu cha utambulisho wa Marekani. Utambuzi kwamba ahadi zetu bado hazijatimia umehamasisha kizazi baada ya kizazi kuchukua hatua za kupigania na kudai kupanuliwa kwa uhuru na usawa kwa watu wote, sio tu ndani ya Marekani, bali duniani kote.”

“Kama tulivyoshuhudia hivi karibuni, demokrasia ya Marekani bado inaendelea kujengeka na kwamba ujenzi wake ni kazi inayoendelea kwamba demokrasia si kituo cha mwisho bali ni safari inayoendelea. Jitihada na urithi wa Martin Luther King zinatukumbusha kuwa kila wakati ni wakati sahihi wa kufanya jambo sahihi.”

Alisema Marekani haiwezi kuogopa au kukataa kupaza sauti dhidi ya ukiukwaji wa haki. Badala yake, kukubali upungufu wake na kuendelea kupigania misingi wanayoiamini ya uhuru na usawa kwa wote na kuendelea kusimama pamoja na wale wanaoamini katika misingi hiyo, ikiwamo Tanzania.

“Ni kwa sababu hiyo, tunaendelea kuchagiza pawapo na maendeleo zaidi na kuenzi kumbukumbu ya Martin Luther King,” alisema.

Habari Kubwa