Bandari Dar yakamilisha ujenzi gati la kuhudumia meli za magari

13Nov 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Bandari Dar yakamilisha ujenzi gati la kuhudumia meli za magari

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekamilisha ujenzi  wa gati maalumu la kuhudumia meli za magari maarufu kama (RoRo) lenye urefu wa mita 327 ikiwa ni sehemu ya maboresho yanayoendelea katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema.

Kadhalika Mamlaka, inaendelea na ujenzi wa eneo la kuhifadhia magari lenye uwezo kuhifadhi magari 7,500 kwa wakati mmoja kwa lengo la kupungumza muda wa kuhudumia meli za magari bandarini hapo.

Hayo yameelezwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Elihuruma Lema, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa lengo la kujenga eneo la kuhifadhia magari karibu na gati hilo ni kurahisisha kazi ushushaji wa magari ili kuongeza ufanisi.

Aidha, amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati hilo Septemba mwaka huu, idadi ya shehena ya magari yaliyoshwa katika gati hilo imeongezeka hadi kufikia 45,000 kwa kipindi cha miezi mitatu tu. 

Amesema kwa mwaka wa fedha 2018/19, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia jumla ya magari 160,000, kutokana na kukamilika kwa ujenzi huo ambao utaongeza ufanisi, imejipanga kuhudumia zaidi ya magari 180,000 kwa mwaka 2019/20.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kuruhusu ujenzi huu wa maboresho ya bandari kwani kukamilika kwa ujenzi wa gati hili la kuhumia meli za magari kumesaidia kuongeza idadi ya shehena hiyo bandarini na kusaidia pia ongezeko la mapato,” amesema Lema.

Amesema hapo awali, Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye urefu wa mita 260 zinazobeba kontena 4,500 lakini mara baada kukamilika kwa maboresho hayo, itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa hadi za urefu wa mita 305 ambazo zina uwezo wa kubeba kontena kati ya 7,000 hadi 8,000.

Kadhalika amesema katika kuhakikisha ulinzi na usalama katika bandari hiyo unaboreka zaidi, wamefunga Kamera maalumu za kiulizi zipatazo 420 kwa ajili ya kudhibiti matukio ya wizi bandarini hapo.

Mbali na uwapo wa kamera hizo, pia wanashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya koboresha ulinzi katika bandari hiyo.

“Kila kinachoendelea kwenye meli tunakiona na kikitokea kitu watu wa usalama wanachukua hatua na kuna ulinzi wa askari wa kwenye maji wanaofanya doria kwa saa 24 katika lango la kuingia bandarini na maeneo yote ya bandari hadi Bagamoyo,” amesema.

Mbali na ulinzi kuimarishwa pia kuna ukaguzi mkubwa wa mizigo ambao hufanywa midaki sita iliyopo bandarini hapo. Amesema kwamba kila Kontena linalopita katika Bandari ya Dar es Salaam linafanyiwa ukaguzi wa kina. 

Habari Kubwa