Bangi yampeleka jela kwa kushindwa kulipa mil. 1.7/-

13Jan 2020
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Bangi yampeleka jela kwa kushindwa kulipa mil. 1.7/-

MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi imemuhukumu mkazi wa Kijiji na Kata ya Mandawa, Wilaya ya Kilwa, Hamisi Mohamedi Mtungata (30), kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh. milioni 1.7 kwa kosa la kumiliki na kusafirisha bangi kilo 14.89.

Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mnyonga Magala, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Magala alimuuliza mshtakiwa kama ana sababu za msingi kutokana na kosa linalomkabili, ambaye aliiomba asipewe adhabu kali kwani ni mkosaji wa kwanza, pia ana familia mke na watoto wawili wanaomtegemea.

Baada ya utetezi huo, Mahakama hiyo alimuuliza Mwanasheria wa Serikali, Godfrey Mramba kama ana kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshtakiwa na kujibu hana.

Aidha, aliomba mshtakiwa apewe adhabu kali kulingana na kosa alilolifanya hasa ikizingatia dawa za kulevya zimekuwa zikiharibu akili za wananchi kwenye jamii.

Hakimu Magala akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 20/2019, kwa kumtaka mshtakiwa huyo kulipa faini ya Sh. milioni 1.7 na akishindwa atumikie kifungo cha miaka mitatu Gerezani.

Hata hivyo, mshtakiwa Mtungata, alishindwa kulipa faini, na kwenda jela kutumikia adhabu hiyo.

Awali, Mramba, aliiambia mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alikamatwa Machi 15, mwaka 2019, na askari Polisi wa Usalama Barabarani waliokuwa eneo la Mitwero akisafirisha bangi hiyo kwenye basi la Kampuni ya Warder lenye namba za usajili T 997 DPL akitokea Mtama kwenda Dar es Salaam.

Habari Kubwa