Barabara zinavyomaliza hazina ya wanyamapori

08Nov 2020
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Barabara zinavyomaliza hazina ya wanyamapori
  • *Kila siku wanahesabu 'misiba' *CAG afukua ushuhuda mpya *TANAPA: Mazito matatu yaja

NI barabara ya lami, kipande cha kilomita 50 ndani ya mandhari wanayoishi wanyamapori, ambayo upitaji wa magari unaibebesha serikali hasara kuu tatu, kiwango cha kuitoa machozi.

Serikali kupitia chombo chake, Wizara ya Maliasili na Utalii, inalalamika kwamba katika kila saa 24, ajali hizo zinasababisha kifo siyo chini ya mnyama mmoja kwenye Hifadhi ya Taifa Mikumi (MINAPA) inakopita barabara hiyo.

Malalamiko hayo yanaenda mbali kwa kugusa pia athari mbaya za kimazingira zinazokinzana na mahitaji ya ustawi wa hifadhi, wakati huo huo MINAPA inabeba mzigo mkubwa wa gharama na ufuatiliaji wa kinachotokea kila siku.

Makene Ngoroma (33), mkazi wa Kitongoji jirani cha Chikwalaza, anayewajibika na uondoaji taka zinazotupwa hifadhini, ana ushuhuda anaouwasilisha kwa simulizi iliyojaa masikitiko, akitamka:

"Ni kawaida hapa kukuta mizoga ya wanyama barabarani wamegongwa na magari... Mimi niko hapa tangu mwaka 2011 nikitokea Moshi, ni mara chache kupita siku pasiwapo mzoga wa mnyama barabarani.

"Inasikitisha kwa kweli, nyani, swala, nyati wanagongwa na mara moja moja twiga na tembo wanagongwa, nyoka pia wanagongwa sana. Wakati mwingine mnyama anagongwa anasagika kama chapati, inakuwa vigumu hata kumtambua."

Ngoroma, ambaye pia ni mwanzilishi wa vikundi vya kuokota taka kwenye hifadhi hiyo, anaendelea kufafanua madhara ya ajali hizo akisema:

"Siyo tu kwamba hupunguza idadi ya wanyama wetu hapa kupitia mauaji ya ajali za barabarani, bali pia huharibu mazingira kwa maana ya miundombinu yenyewe ya barabara na usalama wa eneo hili la hifadhi.

"Gari likishagonga mnyama mfano twiga au tembo, mara nyingi linaanguka au kuvunja baadhi ya vifaa vyake hasa kioo kikubwa cha mbele. Hapo sasa kunakuwa na uchafuzi wa mazingira."

Ili kupata ufafanuzi na mapana ya yanayojiri katika kipande hicho cha Barabara ya Tanzania-Zambia, Nipashe iliamua kumdadisi ofisini kwake Mkuu wa MINAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mathew Mombo, anayeweka sawa kwa mtazamo ufuatao:

"Wanyama kugongwa ni moja ya adha kubwa tunazopata hapa kwenye barabara kuu inayopita ndani ya hifadhi. Ni kweli na ni wazi kabisa kwamba magari yanayopita yanasababisha wanyama wetu kugongwa mara kwa mara.

"Ukweli ni kwamba kama kila dereva angekuwa anatembea kwa mwendo elekezi kwenye eneo hili la barabara, wanyama wasingekuwa wanagongwa. Mpaka unamgonga mnyama, ujue kabisa wewe ulikuwa kwenye spidi ambayo siyo sahihi kwako kupita katika eneo hili, lazima utakuwa zaidi ya 50 au 70 (Km 50 au 70 kwa saa).

"Kwa hiyo, tumekumbana na hilo, wanyama wamekuwa wakigongwa, wakubwa na wadogo na mara kadhaa tumewakamata hao watu kwa sababu akimgonga, sheria zinamtaka asimame, abaki hapohapo.

"Wanapokimbia ajali zikitokea, wanasababisha uharibifu wa mazingira lakini pia wanaua wanyama wadogo watambaao.

"Wanaokamatwa wanapigwa faini ya Sh. 50,000 kwa kuzidisha mwendo na wanaogonga wanyama wanalipishwa faini kulingana na thamani ya mnyama ambaye amegongwa.

"Magari yanayopita hapa ni mengi sana kwa sababu magari yote yanayotoka bandarini kwenda mikoa ya kusini mwa Tanzania na nchi jirani za kusini, lazima yapite hapa. Mabasi yanayopita hapa pia ni mengi mno.

"Wanyama wanaoongoza kwa kugongwa ni wanyama wadogo kama swala na nyani kwa sababu idadi yao pia ni kubwa kulinganishwa na wanyama wakubwa kama tembo, twiga au nyati ambao ni mara chache kugongwa japo mwaka huu tayari kuna twiga amegongwa.

"Mara nyingi na kwa kipindi chote tangu nimekuja hapa, madereva wanaogonga wanyama wakubwa kama twiga, huwa wanakimbia na kutelekeza gari baada ya ajali kutokea. Faini zao zimekuwa zikilipwa na wamiliki wa magari husika."

AONAVYO CAG

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pia ana kilio cha kitaaluma namna sekta hiyo inavyohujumiwa.

CAG Charles Kichere, anayewatambulisha wanyamapori kuwa kivutio kikuu cha watalii, anasikitika kwa kutumia takwimu za kitaifa, kwamba sita kati yao, wanauawa kutokana na ajali za barabarani kila siku.

MINAPA ni kati ya hifadhi za taifa 22, ambayo Mhifadhi Mkuu wake, Mombo, anaitambulisha kwamba inashika nafasi ya tisa kwa ukubwa nchini.

Katika ripoti yake ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma Mwaka 2018/19 iliyowasilishwa bungeni Aprili mwaka huu, CAG Kichere anabainisha kwamba wanyamapori 2,266 waliuawa kwa ajali za barabarani ndani ya mwaka huo wa bajeti.

Ni takwimu zinazobeba ujumbe wa kutoweka wanyamapori 189 kila mwezi, sawa na sita kila siku, jambo ambalo CAG analitafsiri kuwa mwelekeo unaopunguza idadi ya wanyamapori, ambao kimsingi ndiyo mtaji mkuu wa utalii.

CAG anafafanua kwamba tatizo hilo linachagizwa na mamlaka husika kuwa na teknolojia duni katika ufuatiliaji wanyamapori, akigusia kukosekana kamera za barabarani, hivyo kushindwa kutambua wahusika wanaosababisha ajali hizo.

"Mapitio yangu ya Ripoti ya Kitengo cha Ulinzi wa Wanyamapori, yaligundua kuwa katika Hifadhi ya Taifa Mikumi (MINAPA), jumla ya wanyamapori 124 wa aina tofauti, waliuawa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka (Julai Mosi, 2018 hadi Machi 31, 2019).

"Kutokana na idadi hiyo ya vifo vya wanyamapori mbalimbali, MINAPA ilitakiwa kupokea kiasi cha fedha Sh. milioni 56.64 za tozo na adhabu za kusababisha ajali. Hata hivyo, hifadhi hiyo ilipokea Sh. milioni 12.45 tu, sawa na tofauti ya Sh. milioni 44.18.

"Menejimenti ilieleza kwamba ajali nyingi za barabarani zinatokea wakati wa usiku, hivyo kushindwa kuwaona wanaofanya makosa kutokana na kukosekana kwa kamera za ulinzi.

"Vilevile, katika hali nyingine, malipo yalikuwa yanajadiliwa kutokana na ukweli kwamba Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) halina sheria ndogo za kutoza faini na adhabu, ambapo tozo au faini hutolewa kulingana na Kanuni za Taifa za Uhifadhi wa Wanyamapori, ambazo hazimfungi mtu katika mahakama za sheria," anasema.

Nini kifanyike? CAG ana maoni katika ripoti yake kwamba: "TANAPA na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro zitunge sheria ndogo na kuzisimamia ipasavyo.

"Pia, zibuni na kusimamia njia mbalimbali za usalama kama vile kuweka kamera za barabarani, ili kudhibiti ajali za barabarani na hivyo kulinda wanyamapori."

Nipashe iliporejea kwa Mkuu wa Mikumi, Kamishna Mombo, kuhusu hoja kutoka Ripoti ya CAG, alisema bado hazijatekelezwa kwa sababu ununuzi wa kamera ni wa gharama kubwa, wakipendekeza hatua hiyo ichukuliwe na wizara mama.

Vivyo hivyo, alifafanua kwamba mara nyingi wameshindwa kuwanasa madereva wa magari wanaosababisha vifo vya wanyamapori kwa sababu wengi hutoroka baada ya tukio.

Hata hivyo, kuna upande wa pili Kamishna Mombo anakiri kupungua matukio ya ajali kwa sasa, ikiwa ni matokeo chanya ya mkakati wa pamoja na mamlaka nyingine za kiusalama, likiwamo Jeshi la Polisi.

Kamishna Mombo, anayeitaja elimu ya umuhimu wa wanyamapori ndiyo suluhisho la kudumu, anasisitiza mtazamo wao mkuu ni usalama wa viumbe vyao, kuliko mapato yatokanayo na faini za ajali hifadhini, zinazofikia kiwango cha juu Dola za Marekani 15,000 (Sh. milioni 34.456) kwa mnyama kama twiga.

Kwa ujumla, bajeti na taarifa za kiserikali zinafafanua kwamba utalii unachangia robo ya pato la fedha za kigeni, huku pia ni mdhamini wa asilimia 17.5 ya Pato la Taifa, ukitoa pia ajira za moja kwa moja 600,000 na zingine milioni mbili zisizo za moja kwa moja.

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

Kamishna Mombo anasema katika barabara hiyo inayotumiwa na wanaokwenda katika baadhi ya wilaya za Mkoa wa Morogoro, pia takribani mikoa saba iliyoko Nyanda za Juu Kusini, husababisha kila siku magari kati ya 2,500 na 3,000 kupita ndani ya Km 50 hifadhini Mikumi.

Ili kukabili adha ya ajali hizo, anasema wameanzisha kampeni maalum wakishirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilaya za Kilosa na Morogoro, wakiwataka madereva wazingatie sheria za hifadhi.

Anaeleza kuwa kampeni hiyo inafanyika sambamba na uongozi wa hifadhi kuongeza doria za usiku na mchana ili kuzuia ajali ndani ya hifadhi, eneo la kimkakati ambalo watalii wa ndani na kimataifa wanafika kuangalia wanyamapori.

Mkuu huyo wa MINAPA anataja sehemu ya udhaifu wa madereva ni kutozingatia maelekezo kutoka kwenye vibao na alama za tahadhari ya wanyama wanaovuka barabarani zinazojitosheleza kwa ufafanuzi wa kisheria na kiusalama.

Huku akianika sura pana ya mpango mkakati wa kukabili ajali zinazoathiri wanyama na ustawi wa hifadhi kwa ujumla, Kamishna Mombo anatoa angalizo kwamba kutozingatia sheria kunabeba maana ya kuruhusu ajali endelevu zinazoangukia kupungua wanyamapori.

POLISI WANAVYOJIPANGA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, anasema wameshaanzisha utaratibu wa kufanya ukaguzi wa kila mara, kufuatilia utii wa sheria na kanuni miongoni mwa madereva hifadhini.

"Jeshi la Polisi huwa tunafanya doria za mara kwa mara tukishirikiana na watu wa TANAPA pale Mikumi, lile eneo lote tunalifanyia doria ili kuhakikisha madereva wanaendesha kwa mwendo ulioelekezwa kwenye vile vibao.

"Pia, tunatoa elimu kwa madereva kwa kushirikiana na watendaji wa Mikumi, tumekuwa na mpango wa pamoja wa kuwakumbusha madereva kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa kwenye hifadhi na kuchukua tahadhari.

"Wapo madereva wanaozingatia sheria na wapo wakaidi hasa nyakati za usiku, wanaendesha kwa spidi kali na kuua wanyama. Imekuwa shida siyo tu kwa wanyama, bali hata kwa watumiaji wenyewe wa barabara hiyo kwa sababu gari likimgonga mnyama kama tembo, dereva na watu wengine kwenye gari wanakuwa hatarini.

"Walioweka utaratibu za kuzuia spidi kali mle ndani wana maana kubwa. Tunawaasa madereva wafuate sana sheria zilizowekwa ndani ya hifadhi.

"Tumeweka vituo maalum vya ukaguzi ndani ya hifadhi inapopita barabara ndani ya kilomita 50, ili kuwabaini madereva wanaokiuka sheria za usalama barbarani na zile za hifadhi. Tukiwabaini tunawafikisha mahakamani ili wachukuliwe hatua kali," Kamanda Mtafungwa anaonya.

KAULI ZA MADEREVA

Madereva waliohojiwa na Nipashe kutoa neno kwa yanayojiri dhidi yao, wana maoni ambayo kwa ujumla yanashikana mkono na mikakati inayoelekezwa na mamlaka hizo za kiserikali.

Dereva wa basi linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tunduma, Mohamed Hussein, anakubaliana na hatua zilizochukuliwa kiserikali, zikiwamo za elimu hifadhini na ufuatiliaji wa uendeshaji wao.

Mwingine anayeendesha basi kati ya Dar es Salaam na Ifakara, Abbas Shaibu, mbali na kutafsiri kwamba kampeni imekuja kwa wakati mwafaka, anawanyooshea kidole baadhi ya wenzake wanaotumia spidi kali, tofauti na inavyoelekezwa hifadhini, hata kuchangia ajali.

Rai yake ni kwamba zitungwe sheria ndani ya hifadhi zitakazowadhibiti anaowaita 'madereva wakorofi', akiamini hatua hiyo ina nafasi ya kupunguza ajali nyingi katika eneo hilo linalolalamikiwa.

WASIMAMIZI SERIKALINI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dk. John Ndunguru, anataja mkakati wa mkoa ni kudhibiti ajali za wanyamapori na vikwazo vinavyochangia utalii kukwama.

Anasema mkakati huo unahusisha kuweka matatu katika kipande cha Km 50 cha barabara inayopita kwenye hifadhi hiyo ili kudhibiti mwendo wa magari na kutoa elimu kwa madereva na wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda wanyamapori walioko hifadhini Mikumi.

"Upo mkakati mwingine mkubwa zaidi ambao uko ngazi ya kitaifa ambao ni kutengeneza barabara inayopita Mikumi kwenda Kilosa mpaka Dumila ambayo moja kwa moja itapunguza ajali ndani ya hifadhi kwa sababu magari hayatapita tena hifadhini.

"Kikubwa, kila mmoja wetu anapaswa kuthamini manufaa ya Mbuga ya Mikumi siyo tu kwa wananchi wa Morogoro, bali pia Watanzania na dunia kwa ujumla.

"Viumbe waliopo eneo hilo ni adimu, kwa dunia ya leo wamebaki katika maeneo machache ambayo unawakuta katika maeneo yao ya asili," anasema.

Kuhusu hatua zinazochukuliwa kukabili kilio hicho kupitia ngazi ya serikali kuu, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye Baraza la Mawaziri lililopita, Dk. Hamis Kigwangalla, katika ziara yake Hifadhi ya Mikumi, alishaweka wazi tafakuri ya serikali kuona uwezekano wa kubadilisha mwelekeo wa kilomita 50 za barabara, ziwe nje ya hifadhi.

Dk. Kigwangalla alikiri barabara hiyo ya lami haiko katika mazingira rafiki na mbadala mmojawapo uliopo, ni kutoza kodi ya utalii kwa wapitaji.

Alifafanua: "Ni barabara ambayo iko 'bize' sana, ni barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile, hii siyo barabara mahususi kwa ajili ya shughuli za utalii.

"Sisi (serikali) tunatafakari namna ya aidha kuiondoa hiyo barabara au namna ya 'kuwachaji' watu wanaokatiza hizi kilomita 50 ambazo zipo ndani ya Hifadhi ya Mikumi."

Dk. Kigwangalla aliwasilisha takwimu kwamba mwaka 2014 wanyamapori waliogongwa walikuwa 351; mwaka 2015 (361); na mwaka 2016 walikuwa 218.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA (Idara ya Mawasiliano), Paschal Shelutete, alitaja mambo makuu matatu yanayoandaliwa hivi sasa kukomesha tatizo hilo la ajali za barabarani.

Mosi; Kamishna Shelutete alisema mpango uliopo ni kujenga mageti ambayo magari yatasimamishwa kisha madereva na abiria kupewa elimu kuhusu ulinzi na usalama wa hifadhi.

Pili; alielezea mpango wa kamera maalum kwamba sasa uko katika hatua nzuri kwa ajili ya kufungwa kudhibiti uharibifu huo.

Na mwisho; Kamishna Shulutete alisema mpango wa doria uliopo utaimarishwa kwa kiwango bora zaidi ambacho hakitoi nafasi kwa uhalifu huo wa kusababisha ajali zinazozuilika.

Kuhusu hoja ya CAG kwamba TANAPA iwe na sheria ndogo za kuimarisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na wanyamapori kugongwa barabarani, Shelutete anaanika msimamo wao, akisema:

"Adhabu na kiwango cha faini kinachotozwa tunaamini ni kikubwa. Lengo letu siyo kukusanya mapato, bali kupunguza na ikiwezekana kumaliza kabisa ajali za aina hii."

MZIZI WA MIKUMI

MINAPA iliyo chini ya TANAPA, iko wilayani Kilosa mkoani Morogoro, umbali wa kilomita 283 magharibi mwa Jiji la Dar es Salaam na kilomita 311.7 kaskazini mwa Mbuga ya Selous (Hifadhi ya Taifa ya Nyerere), ambayo ni kubwa kuliko zote nchini.

Kwa mujibu wa Kamishna Mombo, Mikumi ni kitega uchumi kilichoanzishwa kisheria mwaka 1964, kikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,070 na baadaye mwaka 1975, serikali iliongezea maeneo yake ya kusini na kaskazini hata kuwa na kilomita za mraba 3,230.

USULI & HISTORIA

Sera ya Wanyamapori ya Tanzania (2007) inabainisha kuwa historia ya uhifadhi wa wanyamapori nchini ilianzia mwaka 1891. Kwa lugha rahisi, ni miaka 129 iliyopita au karne moja na robo.

Hiyo ilikuja kama matokeo ya kuzaliwa kwa sheria za kudhibiti uwindaji zilizoanzishwa na utawala wa Kijerumani uliokuwapo katika zama hizo.

Kwa kurejea sera iliyopo sasa, sheria hizo za awali zililenga kudhibiti uvunaji holela wa wanyamapori; kuhakiki mbinu za uwindaji na biashara ya wanyamapori waliokuwa hatarini kutoweka.

Hifadhi ya kwanza ya wanyamapori nchini ilianzishwa na Wajerumani hao miaka 14 baada ya kutunga sheria katika ukanda wa hifadhi maarufu ya sasa iitwayo Pori la Akiba Selous, mwaka 1905.

Sera inafafanua kwamba kanuni za kitaalamu zilizotumika kuteua maeneo ya hifadhi za wanyamapori, zilizingatia vigezo kama kuwapo wanyama wakubwa pekee na siyo mengine ya ziada yanayotawala sasa, kama makundi yao ya baionuai za kibaiolojia.

Baada ya kupita miaka 16 ya hifadhi kuanzishwa, Tanganyika ikiwa chini ya utawala wa mkoloni mpya, Uingereza, mwaka 1921, kukaanzisha Idara ya Wanyamapori sambamba na mwaka mmoja baadaye, serikali ililitangaza rasmi Pori la Akiba Selous.

Idara hiyo ya wanyamapori ilikasimiwa majukumu ya kiutawala kuhusu usimamizi wa mapori ya akiba, kutekeleza kanuni za uwindaji na kuhakikisha watu na mazao yao hawaingiliwi au kuvamiwa na wanyama.

Sera inafafanua kuwapo historia ya ushuhuda wa hifadhi nyingine mbili kuanzishwa miaka sita baada ya hatua ya mwisho mwaka 1922.

Hapo panatajwa iliyokuwa Bonde Kuu Funge la Ngorongoro (sasa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) na Pori la Akiba Serengeti (sasa Hifadhi ya Taifa Serengeti).

Mnyama Dola                      Sh. milioni

Tembo 15,000                       34. 716

Nyati 1,900                           4.397

Simba 4,900                          11.341

Chui 3,500                             8.1

Twiga 15,000                         34.716

Fisi 550                                  1.273

Ngiri 450                               1.041

Nyani 110                             0.255

Pundamilia 1,200                 2.777

Swala 390                           0.903

Faini wanazotozwa madereva wanapogonga wanyamapori Hifadhi ya Taifa Mikumi (MINAPA). CHANZO: MINAPA, Novemba 6, 2020

Habari Kubwa