Baraza Kuu CUF lajifungia Z’bar

20Mar 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Baraza Kuu CUF lajifungia Z’bar

BARAZA la Taifa la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), jana lilianza kukutana visiwani hapa kujadili mambo mbalimbali kuhusu chama hicho na nchi kwa ujumla.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa kikao hicho katika ofisi zaze zilizoko CUF Vuga, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro, watajadili mambo mazito kwa ajili ya mustakabali wa chama na nchi kwa ujumla.

Alisema kikao hicho pia kitapitia ajenda mbalimbali zilizoandaliwa na kamati ya utendaji kwa mujibu wa katiba ya chama na pia kuzungumzia mambo yanayoendelea nchini hususani hali ya uchumi.

Alisema wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima wahakikishe wanaendelea na kazi nzito ya kuhakikisha serikali inatoa majibu ya msingi kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi.

Aidha, aliitaka serikali kuwahakikishia usalama madaktari ambao watakaokwenda kufanya kazi Kenya kwa kuwa madaktari wa Kenya wameshahoji kitendo cha kupelekewa madaktari hao nchini kwao.

Kuhusu hali ya kisiasa nchini, alisema sio nzuri kwa kuwa shughuli za kisiasa zimepigwa marufuku na vyama vya kisiasa vimewekwa katika wakati mgumu.

Alisema kikao hicho kitapitia ajenda na kufanya maamuzi mazuri kwa maslahi ya kutetea maisha ya Watanzania.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kikao hicho ni halali kwani kilihudhuriwa na wajumbe 42 ambao wanakidhi akidi.

Alisema wajumbe wote wa kikao hicho ni 53, lakini kutokana na sababu za dharura, 11 hawakuweza kuhudhuria.

Habari Kubwa