Baraza la Madiwani laitishwa kukiwa na katazo mkusanyiko

26Mar 2020
Na Mwandishi Wetu
Iringa
Nipashe
Baraza la Madiwani laitishwa kukiwa na katazo mkusanyiko

HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa, imeitisha mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani licha ya kuwapo kwa katazo la mikusanyiko lililotolewa na serikali kukabiliana na maambukizo ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa barua yenye kumbukumbu namba IMC/C.40/23/VO II/188 ya Machi 25 mwaka huu kwenda kwa Mstahiki Meya na wajumbe wa baraza hilo iliyotiwa saini na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Hamis Njovu, wajumbe wote wanatakiwa kuhudhuria mkutano huo.

“Napenda kuwataarifu kuwa mkutano wa Baraza la Madiwani utafanyika Machi 26 mwaka huu, siku ya Alhamisi (leo) kuanzia saa 2:00 asubuhi katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.

“Kwa barua hii, mnaalikwa rasmi kuhudhuria mkutano huo bila kukosa, menejimenti inaomba radhi kwa usumbufu ambao umejitokeza," ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana kuhusu kuitishwa kwa mkutano huo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alidai anachojua kikao hicho kimeitishwa kwa ajili ya kumng’oa Meya wa Manispaa hiyo.

“Tunachoshangaa kuna tishio la corona na ndiyo sababu iliyotumika kuaihirisha kikao cha Baraza la Madiwani jijini Mbeya, hapa kesi ya kupinga kuvuliwa umeya inatolewa uamuzi Machi 27 mwaka huu (kesho) kwamba mchakato wa kumvua uendelee au usiendelee na siku moja kabla, wameitisha kikao cha madiwani na wanataka kumvua umeya.

“Tunashangaa wanataka kufanya kikao hiki, tunachoona serikali haiko ‘serious’ (makini) na corona, tumekubaliana kusiwe na mikusanyiko, lakini wao wanaitisha mkutano ambao ni mkusanyiko," alisema.

Mbunge huyo alisema analazimika kuhudhuria mkutano huo licha ya kuwapo kwa tishio la maambukizo ya corona kwa kuwa asipohudhuria, ataathiri akidi ya chama chake cha Chadema.

Machi 17 mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza uamuzi wa serikali wa kufunga shule za awali, msingi na sekondari na kuzuia mikusanyiko ya mikutano, semina, warsha, makongamano na mikusanyiko mingine ili kujilinda dhidi ya uwezekano wa kusambaa kwa corona.

Habari Kubwa