Bashe akaribishwa na ujumbe mzito

23Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bashe akaribishwa na ujumbe mzito

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga, amemkaribisha Naibu Waziri mpya wa wizara hiyo, Hussein Bashe, kwa kumweleza kwamba jambo la muhimu katika kutekeleza majukumu yake ni kufanya kazi kwa bidii na weledi.

WAZIRI wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza jambo na Naibu Waziri mpya wa wizara hiyo, Hussein Bashe, baada ya kuapishwa jana Ikulu.

Hasunga alisema hayo jijini Dar es Salaam alipoongoza kikao kazi cha uongozi wa juu wa Wizara ya Kilimo ili kutoa taswira ya mwelekeo wa wizara hiyo.

Kikao hicho kilichofanyika kwa saa kadhaa, kilihudhuriwa na Naibu Mawaziri Omary Mgumba na Hussein Bashe pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Mathew Mtigumwe.

Hasunga aliwataka Mgumba na Bashe kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili kutimiza azma ya serikali ya kuimarisha uchumi wa wananchi kadhalika maendeleo kwa ujumla wake.

Alitoa taswira ya mwelekeo wa wizara hiyo katika mipango ya muda mfupi na muda mrefu ili kuwa na weledi na utendaji uliotukuka katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015/2020.

Rais John Magufuli alimteua Bashe kuwa Naibu Waziri wa Kilimo kuchukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye sasa ni Waziri wa Viwanda na Biashara.

Moja ya mambo aliyoyabainisha Hasunga ni pamoja na haja ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazomkabili mkulima na sekta hiyo kwa ujumla.

"Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo na tayari tuko katika hatua za mwisho kwa sababu hatuna sheria na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kupitiwa upya," alisema

Pia alisema sheria zinazotumika kwa sasa ni za bodi za mazao mbalimbali, ambazo pia zina changamoto zake na kuna mazao ambayo hayana bodi kiasi kwamba kuwatetea wakulima wa mazao hayo inakuwa vigumu.

Mazao yaliyo katika utaratibu wa bodi ni pamoja na pamba, kahawa, chai, korosho, pareto na tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Kadhalika ameeleza kuhusu usajili wa wakulima wa mazao yote na bodi hizo ziliagizwa kuwapatia vitambulisho kwa ajili ya kuwatambua wakulima hao na wanapofanyika kazi zao ili iwe rahisi kuwahuduma.

Pamoja na mambo mengine, Hasunga alielezea umuhimu wa Wizara ya Kilimo kuanzisha bima ya mazao itakayokuwa suluhisho kwa wakulima nchini ambao kwa muda mrefu wamekosa utetezi pindi wanapopatwa na majanga kutokana na uchache wa mvua au vinginevyo, jambo linalosababisha kukosekana kwa mazao ya kutosha.