Bashe: nawindwa kuuawa kwa kuundiwa ajali

10Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Bashe: nawindwa kuuawa kwa kuundiwa ajali

HUSSEN BASHE, Mbunge wa jimbo la Nzega Mjini kwa tiketi ya CCM, amedai kuwa ametumiwa ujumbe wa vitisho kuwa yeye ni miongoni mwa watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale watakapoonekana ikiwemo kuundiwa ajali.

Hussen Bashe.

Kauli hiyo ya Bashe aliitoa leo Bungeni wakati akiomba muongozo kwa Naibu Spika ambapo alitaka Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili matukio hayo ya utekaji vinavyotokea nchini.

“Kuna wabunge wengine akiwemo Mbunge wa Geita Joseph Kasheku Musukuma, ambao wamo kwenye orodha ya watu wanaowindwa ili wauliwe”,amesema Bashe.

Bashe amesisitiza kuwa Bunge na Serikali haviwezi kulifumbia macho jambo hilo haramu ambalo kwa sasa imekuwa gumzo katika midomo ya watu masuala ya utekaji watu na kuwapeleka kusipojulikana.

"Kuna watu wamenitumia ujumbe kwamba mimi ni kati ya watu 11 waliopo hatarini kufanyiwa vitu vibaya popote pale tulipo. Bunge na Serikali haviwezi kulifumbia macho jambo hili la haramu wakati Watanzania wanatekwa na watu wasiojulikana". Ameandika Mbunge Bashe kupitia ukurasa wake wa twitter.

Aidha Bashe amesema kuwa kikundi kinachohusika na matukio ya utekaji kiko ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba hao ndiyo waliohusika na tukio la kumteka msanii Roma Mkatoliki.

Habari Kubwa