Bashiru aanika alivyopata taarifa za uteuzi wa JPM

28Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Bashiru aanika alivyopata taarifa za uteuzi wa JPM

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Bashiru Ally, amebainisha alivyopata taarifa za uteuzi wa nafasi hiyo kupitia mitandaoni ya kijamii wakati akijiandaa kufanya kazi maalum za Chama Cha Mapinduzi (CCM), alizopewa na Rais John Magufuli.

 

Balozi Bashiru ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Makuu wa CCM, aliteuliwa juzi na Rais Magufuli kushika nafasi hiyo iliyokuwa wazi baada ya Balozi John Kijazi kufariki dunia katikati ya mwezi huu.

Akizungumza baada ya kuapishwa Ikulu Dar es Salaam jana, Balozi Bashiru alisema hawezi kuzungumza mengi kwa sababu kuu mbili, akizitaja:

"Kwanza ni mazingira ambayo nimepata uteuzi huu. Mheshimiwa Rais ulinipa kazi ambazo kwa ratiba zingechukua mpaka mwezi mzima wa tatu (Machi) na tukaagana na ilikuwa niondoke kesho (leo) au keshokutwa (Jumatatu) kwenda kufanya kazi uliyonielekeza ndani ya chama.

"Jana (juzi) jioni, nikiwa ninasoma mafaili yangu, ninapata taarifa kupitia kwenye mitandao kwamba umeniteua. Mshtuko huo hauniwezeshi kusema mengi, bado ninatafakari sana, nitafanya nini? Nitafanya vipi kukidhi matarajio yako kwa imani uliyonipa kwa mfululizo?"

Balozi Bashiri aliwaomba Watanzania wamwombee ili akidhi matarajio ya Rais katika majukumu hayo mapya.

"Ninamwomba Mungu anisaidie. Sababu ya pili ni mila, maadili, miiko ya kazi hii mpya. Upande mmoja balozi, upande mwingine Katibu Mkuu Kiongozi.

"Kwa mila, desturi, maadili na miiko ya utamaduni wa kazi hizi, siyo kazi ya maneno maneno! Ni za kusikiliza, kujifunza, kuchambua, kuamua na kutenda," alisema.

Balozi Bashiru, mhadhiri wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alimwahidi Rais Magufuli kuwa hatamwangusha, akimwomba Mungu amsaidie.

Aliwaomba viongozi wakuu wa mihimili ya serikali wawe walimu wake na kuahidi kuwa mwepesi wa kujifunza.

"Nilikuwa nikifuatilia maelekezo yako ili tuweze kuyasimamia ndani ya chama kupitia serikali. Yale niliyokuwa nikisimamia na kupeleka kwa Waziri Mkuu, ndiyo hayo nimekabidhiwa leo (jana).

"Kati ya mambo (Rais) uliyosema Dar es Salaam, la kwanza ni umuhimu wa mawasiliano ndani ya serikali na mawasiliano kati ya serikali na umma.

"Tutalisimamia ili kuhakikisha serikali inafanya kazi kama timu moja kupitia utumishi wa umma, lakini pia idara, taasisi, wizara na mamlaka mbalimbali serikalini zinatoa taarifa kwa wakati na kwa usahihi kwa wananchi, ili wananchi wajue serikali yao inafanya nini," aliahidi.

Balozi Bashiru pia alisema Rais Magufuli tangu ameingia madarakani amekuwa akisisitiza umuhimu wa uzalendo, uadilifu na utumishi kwa wananchi hasa katika kutatua kero zao.

"Ninakuahidi nitalisimia hili kwa sababu umelisimamia kwa nguvu zote. La mwisho ni umuhimu wa kusimamia haki na umesisitiza wajibu wa kila mmoja wetu.

"Umezungumzia kodi au tozo mbalimbali, kuhakikisha utaratibu wa kisheria na misingi ya haki inazingatiwa na kusimamia uwajibikaji ili nchi ipige hatua ya kutosha, nitalisimamia.

"Mungu amemchukua Balozi Kijazi lakini ametuachia hazina kubwa. Alikuwa mchapakazi na mpole, siwezi kusema nitakuwa kama Balozi Kijazi, lakini ninamwomba Mungu anibariki niendeleze yale aliyokuwa anafanya katika uongozi wake," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Spika Job Ndugai, Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema chombo hicho kitampa ushirikiano Balozi Bashiru.

"Nikuombe ule ushirikiano ambao tulikuwa  tunauzungumza aliokuwa nao mtangulizi wako, tunautarajia kutoka kwako kwa maana ya kuwa kiungo kati ya serikali na Bunge.

"Tunafahamu mambo mengi kabla ya kuletwa bungeni, yanapita mikononi mwako, tunaamini ushirikiano utaendelea kuwapo," alisema.

Alisema Bunge litaendelea kutoa ushirikiano ambao umekuwapo na kwamba Rais amekuwa akiwaheshimu na wataendeleza ushirikiano huo.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma, alisema amemfahamu Balozi Bashiru kwa muda mrefu kwa sababu siku zote amekuwa mwanafunzi wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi (Rais awamu ya pili), Benjamin Mkapa (Rais awamu wa tatu), Jakaya Kikwete (Rais wa awamu ya nne) na Rais Magufuli.

"Mahakama tunategemea watumishi wa umma, soko letu kubwa la watumishi wa umma linatoka serikali kuu, tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu sana na serikali kuu, laini ya mawasiliano yetu kati ya mahakama na serikali kuu tutaendelea kuiboresha," alisema.

Habari Kubwa