Bashiru afunguka urais Zanzibar

09Jul 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Bashiru afunguka urais Zanzibar

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ameeleza kinachoendelea kuhusu mchakato wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar, huku akiijibu hoja ya wanaodai kwamba mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho hupatikana mkoani Dodoma.

KATIBU Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, picha mtandao

Dk. Bashiru amesema tayari majina matano kati ya 31 ya waliojitokeza kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo yameshapatikana kwa ajili ya mchujo wa vikao vinavyofuata, lakini hayatawekwa wazi kwa umma.

Aliyasema hayo jana kwenye mahojiano ya moja kwa moja na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya vyombo vya habari vya Azam, Tido Mhando, kwenye kipindi cha ‘Uchaguzi 2020’ ambacho ni mfululizo wa vipindi vya uchaguzi.

Majina hayo, kwa mujibu wa Bashiru, yataendelea kuwa siri hadi vikao vya uamuzi vitakapoamua kuyaweka wazi kwa kuwa kanuni za uongozi kuanzia shina hadi taifa zinawaongoza kutotaja siri za vikao.

“Vikao vya ngazi za juu vitakapoamua kwamba hii taarifa itolewe itatolewa lakini kwa sasa itabaki kuwa siri kama kanuni zinavyotuongoza na wale wenye kawaida ya kutoa siri za chama huwa tunawawajibisha kwa sababu wanakwenda kinyume cha utaratibu tuliojiwekea,” alisema.

Alisema mchakato wa kumpata mgombea urais wa Zanzibar huanzia kwa wagombea kuchukua fomu na kisha uteuzi kufanywa na vikao maalum vya Kamati Maalum ya NEC baadaye Kamati Kuu ya chama na kisha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Akizungumzia madai ya baadhi ya watu kuwa rais wa Zanzibar huchaguliwa Dodoma, Dk. Bashiru alisema wanaosema hivyo wanapotosha kwa sababu chama hakimchagui rais bali kinateua mtu atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

“Mchakato wa uteuzi wa mgombea hauwezi kuwa mchakato wa uchaguzi, hivyo ni vitu tofauti. Nadhani mawazo hayo hayawezi kuwa ya wana CCM, hivyo sioni haja ya kuyajadili kwa sababu naamini hakuna mwana CCM mwenye mawazo kama hayo.

“Kila chama kikishateua mgombea wake na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikampitisha kwamba anakidhi vigezo, anakwenda na wenzake wa vyama vingine kupigiwa kura na wazanzibari na siyo raia wengine ambao si wazanzibari,” alisema Dk. Bashiru.

Kuhusu kujitokeza kwa idadi kubwa ya wagombea nafasi ya urais Zanzibar, Dk. Bashiru alisema hiyo ni dalili njema kwamba kuna demokrasia ya kweli kwa ndani ya chama hicho ambayo inataka kila mwanachama awe na haki ya kuchagua na kuchaguliwa.

Alisema si ajabu kujitokeza kwa wagombea wengi wa urais Zanzibar kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa hali imekuwa hivyo hata marais upande wa Bara wanapomaliza muda wao, idadi ya wanaoonyesha nia imekuwa kubwa kila mwaka.

Dk. Bashiru alisema hakuwa na shida ya wingi wa wagombea waliojitokeza Zanzibar bali alitoa angalizo kwa wanaojitokeza kuzingatia taratibu, kanuni na utii kwa chama chao kwa kuwa sifa zao ndizo zinaweza kukiimarisha chama au kukidhoofisha.

Alisema CCM ina uhakika kwamba mgombea itakayemsimamisha atashinda kwa kishindo kwa sababu atakuwa mpya tofauti na vyama vingine ambavyo vitasimamisha wagombea wale wale ambao ni wazoefu wa kushindwa.

Maalim Seif (Sharif Hamad) hawezi kumshinda mgombea wa CCM Zanzibar kwani chama cha ACT Wazalendo kitakachompitisha hakina mtandao mpana wa wanachama huku akisema kuwa atawezaje kama alishindwa akiwa CUF chenye mtandao mkubwa.

Alisema ana uhakika chama hicho kitapata ushindi wa kishindo Zanzibar na Tanzania kutokana na maendeleo makubwa ambayo Dk. Mohamed Shein ameyafanya kwa upande wa Zanzibar na Bara kwa maendeleo ambayo Rais John Magufulia amefanya.

Akizungumzia madai ya Tume Huru ya Uchaguzi (NEC), Dk. Bashiru alisema linajadilika ingawa anaamini kwamba tume za sasa zinauwezo mkubwa wa kuendesha chaguzi hizo kwa ustadi mkubwa.

“Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zina uwezo na uzoefu mkubwa sana wa kuendesha chaguzi huru na haki na mimi sitaki kuamini kabisa kwamba tume hizi hazina uwezo huo na nahimiza tulinde uimara wa tume zetu na kuondoa kasoro ndogo ndogo,” alisema.

Kuhusu kama Bunge lijalo litafanya mabadiliko ili kumwongezea muda mwingine Rais John Magufuli baada ya mwaka 2025 , CCM italipokea jambo hilo kwa mikono miwili, alisisitiza kuwa Rais Magufuli hawezi kukubali mpango huo kwa kuwa atakwenda kinyume cha wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Alisema Rais Magufuli ametimiza ndoto za Mwalimu Nyerere kwa kukamilisha miradi mikubwa aliyokuwa akiipigania kama kuhamia Dodoma na ujenzi wa bwawa la umeme hivyo, hawezi kwenda kinyume naye.

Habari Kubwa