Bashiru aonya wanaoitishia CCM

17Feb 2020
Na Waandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Bashiru aonya wanaoitishia CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema chama hicho hakitasita kumfukuza mwanachama wake bila kujali, umri, cheo au wadhifa kwa kukitishia chama na kuzungumza matatizo katika mitandao ya kijamii badala ya kuwasilisha kwenye vikao vya chama.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, picha mtandao

Alisema CCM ni chama kikubwa nje na ndani ya nchi na kinaheshimu demokrasia kwa wanachama wake hivyo matatizo yanapotokea kati ya viongozi wa chama na wanachama yanapaswa kufikishwa katika vikao halali vya chama badala ya kukimbilia kuandika katika mitandao ya kijamii.

Dk. Bashiru alitoa onyo hilo kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Manispaa ya Morogoro wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho uliofanywa na Mbunge wa jimbo hilo, AbdulAziz Abood, katika kipindi cha mwaka 2015-2020.

Dk. Bashiru, alisema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya siku za hivi karibuni baadhi ya wanachama na wengine waliowahi kuwa viongozi na kushika nyadhifa mbalimbali kukimbilia katika mitandao ya kijamii kueleza matatizo au tofauti zinazotokea ndani ya chama hicho, na kuonya kamwe matatizo hayo hayawezi kujibiwa na yeye katika mitandao ya kijamii.

“Kama kuna tatizo ndani ya chama kwa kiongozi na mwanachama, utaratibu umewekwa mzuri katika chama chetu, peleka tatizo katika vikao kuna ngazi ya tawi, wilaya na mkoa, ukishindwa peleka kwa Katibu Mkuu, lakini sio kukimbilia katika mitandao ya kijamii, hatuwezi kukujibu huko zaidi tutakuchukulia hatua kali ikiwamo ya kukufukuza uanachama,” alionya Dk. Bashiru.

Alimpongeza, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abood kwa kutekeleza ilani ya chama hicho kwa vitendo na kukubarika kwa wananchi wake.

“Nimekuwa nikisikia mengi unayofanya kwa wananchi wako, lakini leo nimeshuhudia mwenyewe mwendelezo huo wa utekelezaji wa Ilani ya chama baada ya kutoa gari la wagonjwa kusaidia wananchi kukimbizwa hospitali ndio tunataka wabunge kama nyinyi inatufanya CCM kutembea kifua mbele,” alisema.

Awali akiwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, Abood alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuleta fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa katika jimbo hilo, ikiwamo ujenzi wa stendi ya kisasa, soko kuu, miundombinu ya barabara, huduma za afya, mradi mkubwa wa maji na huduma nyingine za kijamii.

Alisema ahadi zote alizoahidi wakati wa uchaguzi kwa sasa ametekeleza kwa asilimia 90 na asilimia 10 iliyobaki kwa kushirikiana na wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo na uongozi wa CCM katika wilaya hiyo.

Katika hatua nyingine Dk. Bashiru amewapokea na kuwakaribisha katika chama madiwani wawili wa Chadema, akiwamo wa kata ya Kilakala, Mabura Lusewa na Gabriel Temba, wa Kata ya Kihonda Maghorofani.

Madiwani hao wameeleza wameamua kujiunga na CCM ili kumuunga mkono Rais Magufuli kutokana na kuwaletea maendeleo wananchi.

WANAOANZA KAMPENI MAPEMA KUFYEKWA

Chama hicho pia kimeonya wagombea wa viti vya udiwani na ubunge watakaoanza kampeni kabla ya muda na kutoa zawadi kuwa majina yao yatakatwa.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Philip Mangula, alitoa tahadhari hiyo jana wakati akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati za Siasa za CCM Mkoa wa Shinyanga, kuwa wagombea wote wanapaswa kufuata kanuni na maadili ya chama.

Alisema chama hicho kina kanuni na taratibu zake na kuonya wagombea wote ambao wana nia ya kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, watakaoanza kampeni kabla ya muda watafyeka majina yao.

“Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tunataka taratibu, kanuni na maadili yafuatwe kwenye kugombea nafasi za udiwani na ubunge, wale ambao wataanza kampeni kabla ya muda pamoja na kutoa vizawadi tutafyeka majina yao, msubiri muda ukifika ndipo muanze kujinadi,” alisema Mangula.

“Tunataka nidhamu ndani ya chama na hakuna jamii ambayo haina taratibu namna ya kuishi, hivyo kamati za siasa chungeni sana wagombea ambao wataanza kufanya kampeni kabla ya muda wachukulieni hatua na mkishindwa sisi tutaiwajibisha kamati nzima,” aliongeza.

Pia aliwataka wana-CCM kuendelea kushikamana na kuwa wamoja hasa kwenye kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, pamoja na kuhamasisha wananchi wajitokeze kupiga kura ili chama kipate ushindi wa kishindo kuliko wa mwaka 2015 wakati chama kilivurugika.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, alimhakikishia Mangula kuwa chama kimejipanga vizuri na hakuna hata kiti kimoja watakachokipoteza kuanzia nafasi ya udiwani na ubunge, huku akiahidi kutekeleza maagizo ambayo ameyatoa ikiwamo wagombea kutoanza kampeni kabla ya muda.

Baadhi ya wabunge mkoani Shinyanga akiwamo Ahmed Salum wa Jimbo la Solwa, alimpongeza Rais John Magufuli kwa kazi nzuri ya kutekeleza ahadi nyingi za wananchi kwa asilimia kubwa na wananchi kuendelea kuwa na imani na CCM.

*Taarifa imeandikwa na Ashton Balaigwa (Morogoro) na Marco Maduhu (Shinyanga)

Habari Kubwa