Bashiru awageukia waliorejea CCM

24Feb 2020
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Bashiru awageukia waliorejea CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amewataka wanachama ambao walikihama chama hicho na hivi sasa wameamua kurejea wasiwe chanzo cha kuanzisha makundi ndani ya chama.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, picha mtandao

Amewataka wanachama wa CCM kuwasamehe wanachama hao wanaorejea kwa sababu wamekubali kukiri makosa yao.

Aliyasema hayo wilayani Masasi mkoani Mtwara alipokuwa akizungumza na wanachama wa chama hicho Jimbo la Ndanda na maeneo mengine ya mikoa wa Mtwara na Lindi kwenye hafla ya kumpokea rasmi aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo Chadema, Cecil Mwambe, aliyejiunga na CCM.

“Muwasamehe wanachama wote ambao walikihama chama na hivi sasa wameamua kurejea kwa vile wamekubali kukiri makosa yao,” alisema Dk. Bashiru na kuongeza:

“Lakini kurudi kwao ndani ya CCM kusiwe chanzo cha makundi ndani ya chama, kwa kuwa CCM siku zote haina utamaduni wa kuishi kwa makundi. Aidha na wao wanapaswa kusamehe yote yale waliyoyafanya na kutoruhusu tabia ya uwapo wa makundi.”

Akipokea kadi ya Chadema kutoka kwa Mwambe na kumkabidhi kadi ya CCM, Dk. Bashiru alisema kurejea kwa Mwambe CCM ni wazi kuwa Jimbo la Ndanda linakwenda kukombolewa.

Dk. Bashiru alimtaka Mwambe kurudi na wanachama wengine ambao awali walikuwa CCM, lakini walikimbilia Chadema kwa ajili ya kumfuata mbunge huyo.

Kwa upande wake Mwambe alidai jambo pekee ambalo limemfanya arejee CCM ni namna chama hicho kinavyotekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kila sehemu ya nchi.

Alidai katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa ndani ya Chadema hakuwa na uhuru wa kutoa mawazo yake, hivyo kushindwa kuwatendea haki wananchi wa Jimbo la Ndanda.

Akiwa kwenye ziara katika mikoa ya kusini, Dk. Bashiru alisema kuwa ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa wa Mtwara ukiwamo wa upanuzi wa Bandari ya Mtwara pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini.

Dk. Bashiru alisema licha ya kuridhishwa na miradi hiyo, lakini ipo baadhi ya miradi ambayo inaonekana kutofanywa vizuri kama ilivyokusudiwa katika utekelezaji ambayo ni ujenzi wa barabara pamoja na ukarabati wa uwanja wa ndege.

Alisema miradi hiyo haijatekelezwa vizuri na yeye kama Katibu Mkuu wa chama ameshapokea taarifa ya kusuasua, na taarifa hiyo ataiwasilisha kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli, ili aifanyie kazi.

Alisema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi kupitia ilani yake, hivyo chama kinataka kuona miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.

Habari Kubwa