Bashiru awashtukia watendaji kuficha matatizo ya wananchi

31Jan 2021
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Bashiru awashtukia watendaji kuficha matatizo ya wananchi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameonya tabia ya baadhi ya viongozi nchini, kuficha matatizo halisi ya wananchi pale viongozi wa kitaifa wanapozuru katika maeneo husika.

Amesema kufanya hivyo kunawanyima wananchi haki ya kusikilizwa kero zao na kupata maendeleo.

Dk. Bashiru alitoa onyo hilo juzi, katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, akisema ili kiongozi atatue tatizo, ni muhimu alione kwa macho yake kuliko ilivyo sasa ambapo baadhi ya viongozi katika mikoa na wilaya wamekuwa na tabia ya kutokuweka wazi baadhi ya kero za wananchi, akitolea mfano matatizo ya barabara na maji.

"Tuache maigizo tunafanya kazi za umma, barabara haipitiki, Rais akija aione kwamba haipitiki.

"Kama hakuna maji, siyo mnakwenda kuunga unga maji ya saa 24, baada ya kuondoka yeye tu, yanakatika," Dk. Bashiru alionya.

"Huyu Rais wetu (Dk. John Magufuli) habadiliki, anataka ukweli na kwa chama chetu, msema kweli ni mpenzi wa Mungu na tuna ahadi inayosema 'nitasema kweli daima, uongo kwangu mwiko," alisema.

Vilevile, Dk. Bashiru aliwataka viongozi wa chama na serikali kufika katika kata na vijiji badala ya kuishia mijini.

Mtendaji huyo wa chama aliwaonya wanaotumia  gharama kubwa katika ziara za viongozi huku hali ya wananchi wanaowaongoza ikiwa mbaya.

“Ninawaomba viongozi wa kitaifa na wa mikoa wafanye ziara kwenda chini kwenye matawi na kwenye kata, tuache tabia ya kufanya ziara katika wilaya na mikoa wakati wanachama na uhai wa chama upo katika ngazi ya kata na matawi," alisema.

Habari Kubwa