Bashiru awataka Kinana, Makamba kuacha "utoto"

23Jul 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bashiru awataka Kinana, Makamba kuacha "utoto"

KATIBU Mkuu wa CCM, Bashiru Ally amesema zipo taratibu za kukosoana kwa nidhamu ndani ya chama na kuwataka makatibu wakuu wastaafu Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba kuacha "utoto" kwani ligi iliyotengenezwa sio saizi yao.

KATIBU Mkuu wa CCM, Bashiru Ally.

Aidha amesisitiza kuwa CCM ni chama madhubuti na viongozi wake wapo imara na kuwaonya wanachama wa chama hicho watakaobainika kufanya malumbano ya kirejareja kwa kutafuta kiki za kisiasa watawafukuza.

Hatua hiyo ya Bashiru imekuja baada ya hivi karibuni watu mbalimbali kuonekana wakitoa matamko kufuatia Waraka wa Makatibu Wakuu Wastaafu wa CCM Abdulrahman Kinana na Yusuph Makamba.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa vibanda vya biashara wa CCM mkoa wa Dodoma leo, Katibu huyo amesema kuna taratibu za kukosoana kwa nidhamu ndani ya chama na kuwataka waache "utoto".

"Michezo ya kitoto waachieni upinzani wacheze mchezo wa cha ndimu.Ligi iliyotengenezwa sio saizi yetu mchezo tuliyoachiwa na Mwalimu Nyerere ni kulinda uhuru na kujenga uchumi, hao wanaotutisha sisi hatuwaogopi watu wanaocheza mpira wa cha ndimu maana kocha wao anajificha ndani ya CCM,"amesema.

Ameongeza " Msijifanye majasiri wa kupambana na malumbano waacheni wenyewe wabwabwaje kitoto wataishiwa, ukiona wapinzani wamechangamkia porojo jua wao walioanzisha hawaitakii mema CCM,"

Katibu huyo amesisitiza " Ole wake mwana CCM atakayetumia fursa hiyo ya wapumbavu wa mwaka kulumbana atafukuzwa, hiki ni chama siasa za ukombozi na si za kipuuzi,"

Amesema Mwenyekiti wa CCM(Rais) anawavumilia wanaomtusi na kumkejeli na yupo tayari kuwasamehe lakini sio kwa kufanya hivyo ni uoga.

"Sisi viongozi mzima wa chama chetu ni imara kimfumo, kiitikadi na kiuongozi wapuuzeni hao wapumbavu, hatuogopi kukosolewa hatuwezi kukubali kuitwa majina ya kejeli na watu wasio na shukrani wengine umri wao ni sawa na watoto wake,"amesema.

Amesema "Mimi ni mkurugenzi wa uchaguzi sichokozeki.Mtanzania yeyote makini hawezi kudhubutu kusema CCM kimenuka wanaosema ni wapumbavu kwa kuwa akili ya mwanadamu ya kawaida hawezi kusema hivyo,".