Bashiru aziagiza jumuiya za CCM miradi mikubwa

20Jul 2019
Cynthia Mwilolezi
MANYARA
Nipashe
Bashiru aziagiza jumuiya za CCM miradi mikubwa

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amezitaka jumuiya za chama hicho kubuni miradi mikubwa ya kilimo na viwanda na kuachana na miradi midogo iliyozoeleka ya kupika maandazi na kupangisha.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally.

Aliyasema hayo wakati akishiriki kuvuna mahindi kwenye shamba la Engusero la Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (UWT) Wilaya ya Kiteto, lililowezeshwa na Mbunge wa Viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Martha Umbullah.

Alisema jumuiya za chama hicho zinapaswa kubadilika kwa kubuni miradi endelevu, ambayo itawanufaisha na mwisho wa siku wataondoka katika utegemezi.

"Nashiriki kutekeleza ilani ya CCM kwenye kipengele cha kilimo na viwanda, nina uhakika hili siyo shamba la mtu binafsi, nimeshiriki kuvuna shamba la UWT na Kiteto mmeingia kwenye kumbukumbu yangu," alisema Dk. Bashiru.

Pia, Dk. Bashiru alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, James Ole Millya, kuwa ni mahiri, makini na mchapakazi ndiyo sababu wakakubali kumpokea CCM kutoka Chadema , kwani waliwakataa wabunge watatu wa vyama vya upinzani, walioomba kujiunga na CCM baada ya kubaini kuwa hawawezi kukidhi vigezo vya kuwa wabunge wa chama hicho.

Alisema kwenye Mkoa wa Manyara waliwapokea wabunge wawili wa upinzani Ole Millya na Pauline Gekul wa Jimbo la Babati Mjini (Chadema), ambaye alikuwa mwanafunzi wake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Dk. Bashiru alisema CCM siyo chama cha kuchukua kila mtu, ndiyo sababu waliwakataa hao ambao hata hivyo, hakuwataja majina, akisema kama wangewakubali kuwapokea wote upinzani ungemalizika.

"Tumewakataa wabunge hao watatu waliotaka kuja kwetu kwa kuwa CCM siyo jalala kwa sababu mtu aliyekata tamaa anaweza kujiumiza mwenyewe au kuumiza wenzake," alisema Dk. Bashiru bila kufafanua zaidi kauli hiyo.

Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Manyara, Martha Umbullah, alisema aliipatia UWT Sh. milioni mbili na gharama nyingine za shamba, ili jumuiya hiyo ijiwezeshe kiuchumi.

"Niliona badala ya kuwapatia samaki niwape nyavu wakavue samaki na shamba hilo la mahindi litawasaidia kinamama hawa wa UWT Kiteto katika kujinufaisha kiuchumi,” alisema Umbullah.

Kwa upande wake, Millya alisema miradi mingi ya maendeleo iliyofanyika wilayani Simanjiro kupitia Rais John Magufuli, ndiyo sababu yeye kujiuzulu Chadema na kujiunga na CCM.

Habari Kubwa