Bashiru: Katiba Mpya mchakato, ajenda endelevu

25Feb 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Bashiru: Katiba Mpya mchakato, ajenda endelevu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk.Bashiru Ally, amesema mchakato wa Katiba mpya ni ajenda ya kudumu ya wananchi na haiwezi kufa licha ya kutekwa na wanasiasa wenye uchu wa kuingia Ikulu.

Akijibu swali la mwandishi kuhusu mchakato huo wakati akipokea madiwani 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Jiji la Mbeya waliohamia CCM, Dk. Bashiru alisema kuna watu wanadhani ukiibua mchakato huo inalipa kama ilivyokuwa mwaka 2015.

“Ninawajua watu wavivu wa kufanya siasa za ushindani. Wanatafuta viajenda hivi ambavyo vitawapa kiki. Hii ni ajenda muhimu lakini tumejadili tangu miaka ya 1980 na hii Katiba ya mwaka 1977 tumejadili sana na kuna mapinduzi makubwa yamefanywa ikiwamo kujumuisha haki za binadamu pamoja na mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

“Mwaka 2015 watu walidhani ajenda ile itawapeleka Ikulu wakaidandia Ukawa (Umoja wa katiba ya Wananchi), ajenda ya wananchi kuvishwa na vyama vya watafuta Ikulu ilionyesha mchakato ule ulidandiwa na watu wanaotafuta Ikulu,” alisema.

“Ndio maana hawakupata Katiba mpya wala Ikulu na hili ndiyo kikwazo kikubwa tunapoingia kujadili masuala ya kitaifa, wanasiasa ndio wa kwanza kudandia ikiwamo mimi kwa sababu kwa sasa ni mwanasiasa,” aliongeza.

Alisema jambo la wananchi wanasiasa wanatafuta namna ya kuligeuza na kuwa jambo lao.

“Mchakato ukavunjika wakapanda treni inaitwa Ukawa wakateka ajenda ya wananchi. Ikulu hawakuingia na Katiba haikupatikana. Hiyo Ukawa ingekuwa binadamu haina macho, masikio, miguu na mikono.

“Kama ajenda ya UKAWA ingekuwa ya kudumu si wangeendelea kuwa wamoja? Lakini baada ya Ikulu kugoma ngoma ikagoma ya Ukawa wengine wakaenda ACT, wengine wakabaki CUF ya Lipumba,” alisema.

Alibainisha alipozungumza katika kipindi cha dakika 45 alisema ajenda ya katiba mpya ni ya wananchi na haiwezi kufa kwa sababu ya wanasiasa.

“Kuandika katiba mpya ni mchakato si maudhui, inaandikwa na nani inashirikishaje wananchi, ukisikiliza wanaosema katiba mpya wanasema tume huru, nchi yetu hii ina eneo la ardhi na uhuru wananchi kunufaika na rasilimali ardhi ni jambo kubwa kuliko Tume huru,”alisisitiza.

Habari Kubwa