Bashungwa aagiza kigogo wa TARURA avuliwe madaraka

23Jan 2022
Mary Geofrey
Ruvuma
Nipashe Jumapili
Bashungwa aagiza kigogo wa TARURA avuliwe madaraka

​​​​​​​WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa, amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, kumrudisha makao makuu na kumpangia kazi nyingine aliyekuwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Ibrahim Kibasa.

Meneja huyo alishindwa kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara mkoani Ruvuma mwaka 2020.

Bashungwa alitoa maelekezo hayo jana wakati akikagua ujenzi wa Daraja la Ruhuji lenye urefu wa mita 22 na upana wa mita nane lililoko katika barabara ya Mabatini – Ramadhani.

Daraja hilo linaunganisha Kata za Njombe Mji na Ramadhani katika Halmashauri ya Njombe Mji, mkoani Njombe.

Waziri Bashungwa alisema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja hilo ambalo lilianza kujengwa Mei 21, 2020 na lilitakiwa kukamilika Septemba, 2020.

“Kuna uzembe mkubwa katika ujenzi wa daraja hili ambalo ni kiungo muhimu kwa wananchi wa maeneo haya kwa kuwa wanatumia daraja hili kwa ajili ya kusafirisha mazao yao sokoni, hivyo kususua kwa ujenzi wa daraja hatuwatendei haki wananchi” alisema Bashungwa.

Bashungwa alimwagiza Meneja TARURA Mkoa wa Njombe, Mhandisi Gerald Matindi, kumsimamia mkandarasi anayejenga daraja hilo na kuhakikisha anakamilisha kwa wakati.

Waziri Bashungwa pia alitoa muda wa miezi sita kwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Njombe kutatua matatizo ya miundombinu katika mkoa huo.

Akiwa katika Kijiji cha Mbalache wilayani Makete, Bashungwa aliagiza kuanza haraka kwa ujenzi wa Barabara ya Lupila – Kipengere yenye urefu wa kilometa tano kwa kiwango cha changarawe na kutoa wiki mbili mkandarasi kuanza ujenzi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiongezea TARURA bajeti kutoka Sh. bilioni 8.4 mwaka 2020/21 hadi Sh. bilioni 22.5 mwaka 2021/22.

Habari Kubwa