Bashungwa, Aweso wamwakilisha Samia kusikiliza, kutatua kero

20May 2022
Gwamaka Alipipi
DAR
Nipashe
Bashungwa, Aweso wamwakilisha Samia kusikiliza, kutatua kero

WAZIRI wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wamekutana na makundi mbalimbali kusikiliza kero zao zinazowasibu, kisha kuzitolea ufafanuzi zile zilizopo kwenye uwezo wao na zingine kuzipeleka eneo husika.

Mawaziri hao kupitia mkutano maalum uitwao ‘Sema na Mama’ walikutana na makundi hayo baada ya agizo la Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Tabora.

Makundi hayo ni watu wenye ulemavu, waendesha bodaboda, wajasiriamali na wamachinga wanaofanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali Mkoa wa Tabora.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Donatus Rupoli, ambaye ni mlemavu wa macho, alitaka watoto wa wenye chngamoto hiyo, kupewa kipaumbele katika ajira kama inavyofanyika sasa kwa wenye ulemavu.

Rupoli amesema wapo wenye ulemavu ambao kutokana na umri mkubwa hawawezi kuajiriwa na badala yake wapewe fursa hiyo watoto wao.

Kadhalika, alisema watu wenye ulemavu waondolewe kodi kutokana na hali zao ambazo zinawafanya watumie fedha nyingi zaidi kuliko wale wasio na ulemavu na kwamba kuondolewa kodi kutawapa ahueni na kupiga hatua katika biashara zao.

Mwenyekiti wa wamaachinga Mkoa wa Tabora, Zubery Omary aliomba kuboreshwa kwa miundombinu katika maeneo waliyotengewa ili mazingira ya kufanyia kazi yawe mazuri zaidi.

BASHUNGWA

Akijibu kero hizo, Bashungwa alikiri watu wenye ulemavu kuwa na umuhimu wa kupata mafunzo ya kompyuta na watoto wa wazazi wenye ulemavu kifikiriwa kupewa kipaumbele katika ajira ambayo ameyachukua kuyafanyia kazi.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuwasaidia wenye ulemavu lakini tatizo ni wao kutumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wasiyo waaminifu, jambo ambalo linaleta shida.

Kadhalika, alisema atawaagiza viongozi wa TBS na Shirika la Viwanda Vidogo vidogo(SIDO) kwenda mkoani Tabora kuonana na mkuu wa mkoa huo ili kuratibu mchakato huo.

WAZIRI AWESO

Waziri Aweso, aliwaahidi kundi hilo kuwanalo pamoja kwamba changamoto zoto zinazowakabili watazitatua.

Alisema changamoto kubwa kwa vijana na makundi maalum ni mitaji na kuwaahidi Serikali itashughulikia huku akiwatoa hofu kwa wao viongozi vijana wamepata dhamana kubwa ndani ya Taifa hivyo, hawatawaangusha katika utekelezaji wa majukumu yao.

Habari Kubwa