Bavicha yalipa somo Jeshi la Polisi

20Mar 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Bavicha yalipa somo Jeshi la Polisi

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), Wilaya ya Shinyanga Mjini, limelitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumika kisiasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao.

Sambamba na kulipa somo jeshi hilo, Bavicha imelitaka kutekeleza majukumu yake ya kulinda usalama wa raia na mali zao.

Kwa mujibu wa baraza hilo, kwenye uchaguzi uliopita ukiwamo uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ule wa marudio katika kata na majimbo mbalimbali, jeshi hilo lilionekana kutumika kisiasa na hasa kwa kuonea vyama ya upinzani na kukibeba chama tawala (CCM) ili kipate ushindi kwa nguvu zote.

Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Shinyanga Mjini, Samson Ng’wagi, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari juu ya hali ya kisiasa nchini pamoja na kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

“Tunaliomba Jeshi la Polisi lisitumike kisiasa na kukipendelea chama tawala bali lifanye kazi yake ya kulinda amani na lisiwe sehemu ya chanzo cha vurugu. Lituache sisi wanasiasa tushindane kwa hoja majukwaani,” alisema Ng’wagi.

“Sisi Chadema huwa tunachukizwa sana pale tunapoliona jeshi letu ambalo ndiyo tunalitegemea kulinda usalama wa raia kuwa sehemu ya wanasiasa. Tunatoa wito kwao wasitubague watu wa upinzani ikiwa sisi sote ni Watanzania na wasimamie amani ya nchi iendelee kutawala hasa kwenye kipindi hiki cha uchaguzi,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, aliwashauri viongozi wa serikali wakiwamo wakuu wa wilaya, kufuata maagizo ya ugawaji wa vitambulisho vya machinga kwa kutolewa kwa wale wafanyabiashara wenye mitaji ya Sh. milioni nne na si kuanza kuonea wafanyabiashara wenye vipato vidogo na kuwadidimiza kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Kahama, Jackson Tungu, alitoa wito pia kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu ambao wamekuwa wakitishia maisha ya viongozi mashuhuri kupitia mitandao ya kijamii, ili nchi iendelee kutawaliwa na amani.