BAWACHA Njombe wamuomba Samia kuingilia kati wabunge 19 waliofukuzwa

28Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
BAWACHA Njombe wamuomba Samia kuingilia kati wabunge 19 waliofukuzwa

Baraza la wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Njombe, wametoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati suala la kuondolewa Bungeni kwa wabunge 19 wa Viti Maalum, wanaodaiwa kuwa wanatokana na chama hicho ili hali wamefukuzwa uanachama.

Wito huo umetolewa na baraza hilo wakati wakizungumza na vyombo vya habari katika mkutano wao uliofanyika mkoani humo.

Mwenyekiti wa baraza la wanawake wa chama hicho Jeni Mgeni na wa wilaya ya Njombe Levina Wikechi ni mwenyekiti wa baraza la wanawake wa chama hicho kata ya Ramadahani, wanasema wao hawawatambui wabunge hao huku wakimuomba Rais kuondosha wabunge hao ili kuimarisha uongozi wake.

“Sisi tunazidi kujiuliza hivi Ndugai yuko pale kwasababu gani na hatuwezi kuamini anavyooendelea kukaa nao pale bungeni na anaahidi kuwalinda kabisa,tunaomba Rais askie kilio cha sisi wanawake wenzake ambao hatupendi kuona katiba inavunjawa wazi,” wamesema.

“Kutokana na matamkoa ya Rais wa sasa ninaamini demokrasia itakaa vizuri na hawa wabunge walioenda bila utaratibu wa Chama naamini anaweza akaliweka sawa.Na sisi tunachokitaka zaidi kwa Rais wetu tuanomba kwanza tume huru lakini pia mabadiliko ya katiba,” amesema Mgeni.

Katibu wa BAWACHA Mkoa wa Njombe, Siglada Mligo, amesema Rais ana mamlaka yote kisheria kuingilia kati mhimili wowote unapokwenda kinyume na sheria hivyo anaamini anaweza kulishughulikia swala hilo la wabunge 19 wanaodaiwa kuto kuwa na vyama huku wakiendelea kutia doa demokrasia na utii wa sheria.

“Rais kwa mujibu wa katiba ana mamlaka ya moja kwa moja kuingilia mhimili wowote pale unapokwenda kinyume na sheria,kwa hiyo ana uwezo mkubwa wa kutoa amri pale atakapojiridhisha wale wabunge 19 wapo pale kinyume cha sheria na katiba,naamini anaweza kushughulika nao kwasababu amekuja kwa mpango wa Mungu,” amesema Mligo.

Amesema anashangazwa kuona kiti cha spika kinaendelea kuwalinda wabunge hao ili hali mwaka 2017 walio kuwa wabunge wengine akiwemo Sophia Simba (CCM) alifukuzwa uanachama na ubunge ukakoma lakini pia mwaka huo huo wabunge viti maalum 8 walifukuzwa uanachama na Chama Cha CUF chini ya mwenyekiti wao Lipumba na ubunge wao ukakoma,inakuwaje wabunge hao 19 waliofukuzwa uanachama wa Chadema kushindikana kupndolewa bungeni.

“Mwaka 2017 kuna mbunge wa CCM Sophia Simba alifukuzwa na Chama chake na Spika wa Bunge Jobu Ndugai alitoa taarifa bungeni na ubunge wake ukakoma.Lakini ilivyokuja kwa CHADEMA kuwafukuza uanachama wanachama 19,spika wa bunge huyo huyo ameahidi kuwalinda,” amesema.

Aidha wameeleza kuwa Chama hicho bado kipo imara na kinaendelea na shughuli zake huku wakitoa rai kwa wanachama kuendelea kuwa wavumilivu na kusikiliza viongozi wao wanasema nini.

Waliofukuzwa uanachama ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga na Tunza Malapo.

Wengine ni Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.