Bei mafuta ya petroli, dizeli zapaa

05May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Bei mafuta ya petroli, dizeli zapaa

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza kuongezeka kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli pamoja na taa yanayopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia leo Jumatano Mei 5, 2021.

Mabadiliko hayo ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.

Bei ya rejareja ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeongezeka kwa Sh46, Sh43 na Sh94 mtawaliwa kwa kila lita moja ya mafuta itakayonunuliwa ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita.

Hiyo ikiwa na maana kuwa sasa wakazi wa jiji la Dar es Salaam watanunua lita moja ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa Sh2,169, Sh2,038 na Sh1,957 kutoka Sh2,123, Sh1,996 na Sh1,863 mtawaliwa waliyokuwa wakinunua mwezi uliopita.

Wakati huo bei za jumla za mafuta hayo zimeongezeka kwa Sh45.97, Sh42.40 na Sh93.33 kwa kila lita ya mafuta itakayonunuliwa.

Katika mikoa ya Kaskazini yaani Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, bei za jumla na rejareja ya petroli na dizeli zimeongezeka Sh90, Sh174 huku bei za jumla zikiongezeka kwa Sh90.2 na Sh173.71 mtawaliwa kwa kila lita moja.

Kwa wakazi wa Arusha sasa watanunua lita moja ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa Sh2,302, Sh2,255 na Sh2,051 kutoka Sh2,211, Sh2,081 na Sh2,051 waliyonunua mwezi uliopita.

Mtwara, Lindi na Ruvuma bei zimeongezeka kwa Sh147 na Sh42 kwa lita kwa kila mnunuzi wa rejareja anaponunua bidhaa hiyo huku wanunuzi wa jumla wakitakiwa kuongeza Sh146.37 na Sh41.78 kwa kila lita mtawalia.

“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo kama ilivyokokotolewa na kanuni iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 656 la tarehe 21 Agosti 2020.”

“Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja. Adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Habari Kubwa