Bei ya mafuta nchini kushuka Juni Mosi

09May 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bei ya mafuta nchini kushuka Juni Mosi

Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza mkakati wa kubana matumizi ya Serikali katika bajeti ya matumizi ili kupata fedha za kupunguza makali ya ongezeko la bei ya mafuta linalosababisha kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 9, 2022 katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari akisema Serikali imesikia kilio cha wananchi cha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

“Katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu tutachukua hatua mbalimbali za kikodi kuweka ahueni kwa wananchi.

“Hata hivyo, kutoa nafuu za kupanda kwa bei za mafuta hakuwezi kusubiri hadi mwaka huu wa fedha, nimeamua kwa hiyo wananchi waanze kupata nafuu kuanzia tarehe Mosi Juni.

Nimeelekeza kwamba, Serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka kwenye matumizi ya kawaida ya Serikali ili ziende kutoa nafuu za bei ya mafuta kuelekea mwaka wa fedha,” amesema Rais Samia.

Amemwagiza Waziri wa Nishati kutoa ufafanuzi kesho bungeni kuhusu hatua hiyo, huku akimwelekeza Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kutoa ufafanuzi wa kodi katika mafuta.

 

Habari Kubwa